SERIKALI wilayani Muheza mkoani Tanga imepiga marufuku shule zote za msingi na sekondari wanafunzi kufanyishwa mitihani siku za ibada ikiwamo Ijumaa, Jumamosi na Jumapili, anaandika Mwandishi Wetu.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Muheza, Mwanasha Tumbo katika hotuba yake ya kufunga sherehe za makambi katika kanisa la Waadiventista Wasabato mtaa wa Michungwani wilayani hapa.
Tumbo ametoa agizo hilo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa Mchungaji wa Kanisa hilo, Laulent Fungomeli kwamba watoto wao wanashundwa kufanya ibada kwa kuwa wanakuwa shuleleni kwa ajili ya mitihani siku za Jumamosi.
Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa shule zote za msingi na sekondari ni marufuku kufanya mtihani siku za ibada ikiwamo Ijumaa,Jumamosi na Jumapili.
Amesema kuwa lazima wanafunzi wafanye ibada kanisani ili kujenga taifa lenye msingi bora wa maadili wa kujua dini huku akiwataka wazazi kusimamia watoto wao katika elimu hasa watoto wa kike.
Amewataka waumini hao kudumisha amani pamoja na kumuombea rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwa kuwa kazi anayofanya ni kubwa ya kutumbua majipu.
Leave a comment