January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DC Makonda abanwa kortini

Spread the love

PAUL Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, amebanwa kwa maswali na Wakili Peter Kibatala anayemtetea, Saed Kubenea, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hali Halisi Publishers Ltd na pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo. Anaandika Happyness Lidwino.

Makonda ambaye ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), aliulizwa maswali baada yua kutoa ushahidi wake mbele ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuhusiana na kesi ya jinai iliyofunguliwa na Desemba mwaka jana baada ya viongozi hao wawili kugombana kwenye kiwanda kimoja jijini.

Ikiwa ni siku ya Makonda kujitetea katika kesi inayosikilizwa na Hakimu Thomas Simba, Wakili Kibatala alimuhoji kwanini aliamua kupeleka kesi hii mahakamani?, Makonda alikaa kimya.

Baada ya Makonda kukaa kimya, hakimu Simba alimwelekeza Wakili Kibatala kuuliza swali la pili, Ndipo Makonda alipoulizwa na wakili, alichukua muda gani kwenda katika gari yake baada ya Kubenea kuanza kumtolewa lugha ya matusi?

Makonda aliieleza mahakama kwamba alitumia muda wa dakika 15, Wakili Kibatala alimuhoji Je, katika dakika hizo hakujibu matusi kutoka kwa Kubenea?

Makonda alijibu kwamba, katika muda huo hakumjibu chochote Kubenea, jibu ambalo, Wakili Kibatala alilitumia kumbana, inawezekanaje katika muda huo Makonda asizungumze kitu?

Hata hivyo, hakimu alimtaka Wakili Kibatala kuuliza swali lingine ambapo aliuliza je, polisi waliokuwa katika eneo la tukio walichukua hatua gani?

Makonda: Polisi walichukua hatua ya kumkamata Kubenea baada ya kuendelea kutoa lugha ya matusi.

Wakili Kibatala alimuuliza Makonda, nani aliyetoa amri polisi wamkamate Kubenea, Makonda alikana na kudai kuwa si yeye isipokuwa polisi ndio walimkamata.

Wakili Kibatala alimuuliza Makonda, “Je, unayajua majukumu ya Mbunge? Je ulijibizana na Kubenea eneo la tukio? Je, unajua ni vigezo gani vilitumika kukuchagua kuwa Mkuu wa Wilaya? Je unafahamu maana ya neno mjinga na mpumbavu?

Maswali hayo ya mtego yalionekana kumpandisha hasira Makonda kutokana na majibu yake kuwa mafupi na kutomridhisha wakili.

Hata hivyo, hakimu aliingilia kati na kumtaka wakili kubadilisha namna ya kuuliza maswali hayo. Hata Wakili Kibatala baada ya kushauriwa na hakimu kubadilisha maswali, aliieleza mahakama kwamba amemaliza.

Makonda alifika mahakamani hapo leo kutoa ushahidi wake huku akifuatiwa na shaidi wake ambaye ni Askali Dc Gabriel mwenye namba F4829 kutoka katika Kituo cha Magomeni.

Kesi hiyo iliyotokana na tukio la 14 Desemba mwaka jana, wakati Makonda na Kubenea, walipokutana kwenye Kiwanda chya nguo cha TOOKU kilichopo Ubungo, ambapo Kubenea alitangulia kufika baada ya kuitwa na wafanyakazi kwenda kusikiliza malalamiko yao dhidi ya menejimenti ya kiwanda.

Upande wa mashtaka unaendelea kutoa ushahidi.

 

error: Content is protected !!