May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DC Kongwa aonya wapotoshaji chanjo ya Korona

Spread the love

 

MKUU wa Wilaya ya Kongwa (DC), mkoani Dodoma, Remidius Emmanuel, amesema atachukua hatua dhidi ya watu watakaotoa taarifa ya upotoshaji kuhusu chanjo ya Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19). Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Emmanuel ametoa onyo hilo leo Jumamosi, tarehe 14 Agosti 2021, akizungumza na wananchi wa Kata ya Mkoka, mkoani humo, katika zoezi la ugawaji wa kadi za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kongwa amesema, atawachukulia hatua za kisheria wale wanaopotosha kwamba chanjo inayotolewa na Serikali, ina madhara kwa binadamu, wakati si kweli.

“Kwa kweli naomba niseme wazi hapa, kuwa Serikali ya Wilaya hii ya Kongwa, sisi kama viongozi kamwe hatutawaonea aibu wale ambao kazi yao ni kuwapotosha watu, kuwa chanjo hiyo ina madhara. Hatutasita kuwachukulia hatua za kisheria,”amesema Emmanuel.

Emmanuel amewaagiza viongozi wa Serikali za mitaa wilayani humo, kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaopotosha jamii kuhusiana na chanjo hiyo.

Ametoa agizo hilo akidai kwamba, kumekuwepo na upotoshaji unaotolewa na baadhi ya watu hasa katika mitandao ya kijamii, kuwa chanjo hiyo ina madhara pindi utakapochanja.

Amesema chanjo hiyo ni hiari hailazimishwi mtu yoyote kuchanjwa, hivyo hakuna sababu ya kuwashawishi walio tayari kuipata, wasijitokeze.
“Ninawaagiza viongozi wangu mlio chini yangu, chukueni hatua za kisheria kwa wanaopita huko na huko wakitoa taarifa kuwa, chanjo hii ina madhara kwa wanadamu,”amesema.

Aidha, amewataka wataalamu wa afya waliopo kwenye vituo vya afya, zahanati na hospitali, pamoja na viongozi wa Serikali na dini, kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili walio tayari waweze kushiriki kupata chanjo hiyo.

error: Content is protected !!