July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DAWASA yawaita wakazi Buza iwaunganishie maji

Spread the love

 

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) nchini Tanzania, imewaomba wananchi wa Mtaa wa Amani, Kata ya Buza kujitokeza kwa wingi kuunganishiwa huduma ya maji safi na salama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ni baada ya kukamilika kwa mradi wa maji Jet-Buza.

Wito huo umetolewa na Mhandisi Sijapata Athuman wakati wa mkutano wa hadhara wa wananchi wa Mtaa wa Amani wenye lengo la kuwaelemisha juu ya huduma mbalimbali za Mamlaka na kuwahamasisha kujiunga na huduma ya majisafi.

“Ni muda wa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata maji ya DAWASA, Serikali kupitia DAWASA imewekeza fedha nyingi katika mradi huu ili kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani basi tuitumie fursa hii kuweza kuungwa na huduma,” amesema Mhandisi Sijapata.

Naye Afisa Huduma kwa Wateja wa DAWASA, Eva Kessy amewaeleza wakazi hao kuwa DAWASA ipo kuwahudumia muda wote na hivyo wasisite kujitokeza pale wanapopata changamoto yeyote kuhusu huduma ya majisafi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Amani, Omar Katoto amewasisitiza wananchi wa mtaa huo kuitumia fursa iliyotolewa na DAWASA ya kupata majisafi kwa mkopo.

“Awali wapo waliolalamika kuwa gharama za maunganisho ni kubwa lakini sasa tumeambiwa huduma tutaipata kwa mkopo, hii ni fursa ya sisi sote kuungwa na maji ya DAWASA,” ameeleza Katoto.

Hivi karibuni, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema wamejipanga vyema kuhakikisha kila mkazi wa Dar es Salaam na Pwani wanapata huduma ya maji safi bila kikwazo na wananchi watapata maunganisho ya maji kwa mkopo.

“Nimetoa maelekezo kwa watumishi wenzangu kuwa maunganisho ya huduma ya maji kwa wateja kwa mara ya kwanza yatakuwa kwa mkopo. Kwa hiyo wananchi wachangamkie fursa hii,” alisema Mhandisi Luhemeja, katika mahojiano maalumu kwenye kipindi cha Twende Pamoja kinachorushwa na Televisheni ya Chaneli 10

Huduma ya Majisafi huambatana na sheria na miongozo mbalimbali inayoongoza utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi hasa ikiwataka kulinda na kuhifadhi miundombinu ya maji.

Ezekiel Lwenge, Mwanasheria wa DAWASA alitoa elimu juu ya Sheria ya maji namba 5 ya mwaka 2019 akiainisha makosa mbalimbali na adhabu zake pale wananchi wanapozikiuka.

Kwa upande wa wanufaika wa Mradi huu, Miriam Jumaa amesema wanafuraha kubwa kufikiwa na huduma za DAWASA na wapo tayari kujiunga nazo kwani zina unafuu mkubwa kwao.

“Mradi huu kwetu ni neema kubwa, gharama za maisha zitapungua kwani maji haya ya DAWASA ni ya bei nafuu kabisa, nipende kuwaomba DAWASA waongeze kasi katika maunganisho kwa wateja wapya ili watu wasikae muda mrefu kusubiri huduma” ameeleza Miriam.

Mradi wa maji Jet – Buza unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.2 utanufaisha takribani wakazi 176,000 katika maeneo ya Yombo, Vituka, Buza, Makangarawe, Machimbo, Sigara, Mji mpya, Kivule, Mwanagati, pamoja na mashine namba 5 ya maji.

error: Content is protected !!