May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DAWASA yaipiga jeki Pugu Sekondari, yatoa ahadi zaidi

Spread the love

 

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa msaada wa kompyuta mpakato tatu zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 2 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu Shule ya Sekondari Pugu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ni hatua ya kuthamini na kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha upatikanaji wa elimu bora nchini.

Kopyuta hizo zimekabidhiwa jana Ijmaa tarehe 6 Mei 2022 na Meneja Mawasiliano DAWASA, Everlasting Lyaro kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii wa DAWASA.

Everlasting alisema kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii Mamlaka hutenga fedha kwa ajili ya kusimamia na kuratibu shughuli za maendeleo na hivyo kupelekea kuwezesha wanafunzi wenye ulemavu kupata nafasi ya kujifunza katika mazingira wezeshi.

Aidha, Everlasting alitoa wito kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Pugu kutunza vifaa hivyo ili viweze kuwasaidia wao pamoja na wanafunzi wengine.

Everlasting alitumia fursa hiyo kutoa ahadi kuwa DAWASA itaendelea kutoa ushirikiano zaidi kwa shule hiyo kongwe nchini ambayo Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifundisha wakati huo ikiitwa St. Francis kabla hajaingia kwenye harakati za kisiasa.

“DAWASA inatoa wito kwa wanafunzi kuvitunza vifaa vilivyotolewa ili viweze kusaidia wanafunzi wengine na kuleta ufanisi uliokusudiwa,” alisema Everlasting.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu, Jovinus Mutabuzi aliishukuru DAWASA kwa msaada huo ambao utaenda kuboresha na kuongeza kasi ya utoaji elimu maalumu ambayo inatolewa mahususi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Pia, alichukua nafasi hio kushukuru DAWASA kwa huduma ya maji wanayopata baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Pugu-Gongo la Mboto ambao umetatua kwa kiasi kikubwa changamoto ya maji shuleni hapo na kumaliza tatizo la magonjwa ya mlipoko yaliyokuwa yakiwapata zamani kutokana na ukosefu wa majisafi na salama.

“Tunashuru kwa msaada huu ambao utaenda kusaidia walimu na wanafunzi kuboresha utoaji elimu kwa wanafunzi wetu wenye mahitaji maalumu kama kuchapa notisi za wanafunzi ambao hawana uwezo wa kuandika” alosema Mutabuzi

Naye, Mwalimu wa elimu maalumu na Mlezi wa Klabu ya Usafi na Mazingira DAWASA, Adrew Cheyo aliishukuru kwa msaada huu ambapo amesema utaenda kuongeza ufanisi katika kutoa elimu.

Pia, alichukua nafasi hiyo kuomba msaada wa bima ya afya kwa wanafunzi pamoja na mahitaji mengine ya muhimu maana uhitaji bado ni mkubwa mno.

“Kama mwalimu wa elimu maalumu msaada huu utatusaidia sana katika kutimiza majukumu yetu katika kuwapa elimu wanafunzi hawa” alisema Cheyo.

Kwa upande wake, muwakilishi wa wanafunzi Innocent Cosmas alisema wanashukuru kwa msaada na utachangia katika kujifunza vitu mbalimbali ikiwemo sayansi na teknologia mpya na amewasihi wanafunzi wenzake kufanya matumizi sahihi na kutunza vifaa hivyo ili viwafae kwa mda mrefu.

Shule ya sekondari Pugu ni moja ya shule yenye klabu ya Usafi na Mazingira inayosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) ambapo kupitia klabu hizo wanafunzi wanapata elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira ili kulinda vyanzo vya maji na utunzaji wa miundo mbinu ya maji.

error: Content is protected !!