September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dawasa wakabidhiwa miradi 341, Prof. Mkumbo awapa heko

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo akikabidhiana mkataba wa Bohari Kuu ya Maji na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja

Spread the love

WIZARA ya Maji nchini Tanzania, imeipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), kwa kushughulikia matatizo ya maji kwa wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)

Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya Bohari Kuu ya Maji, miradi mikubwa 19 na miradi midogomidogo 322 kutoka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuanza kuhudumiwa na Dawasa.

Pia, ilisainiwa mikataba ya makabidhiano ya miradi ya maji, bohari ya maji na kusaini mkataba wa kuhamisha mikataba ya wakandarasi kutoka Ruwasa kwenda Dawasa.

Profesa Mkumbo alisema jitihada zinazofanywa na Dawasa katika kutatua changamoto mbalimbali za maji ana imani, miradi hiyo hawatoshindwa kuisimamia.

Alisema, Serikali ya Tanzania imeamua kuikabidhi bohari kuu ya maji iliyopo ambayo awali ilikuwa inatumiwa na serikali ili iweze kuwa chini ya Dawasa.

“Kwa sasa bohari hii ya maji itakuwa chini ya Dawasa, awali ilikua inatumika na Serikali kununua vifaa na dawa ila toka kuanzishwa kwa Mamlaka za maji vijijini wamekuwa wananunua wenyewe na kutokufanya kazi,” alisema.

Profesa Mkumbo alisema, kwa sasa Dawasa, wanafanya kazi vizuri kwani malalamiko kutoka kwa wananchi yamepungua kwa sehemu kubwa ambapo baadhi ya maeneoyaliyokuwa hayana huduma ya maji yamepata.

Mtendaji mkuu huyo wa wizara ya maji alisema, jumuiya za maji 68 wanazokabidhiwa wakazitendee haki na miradi yote lazima watoe taarifa kwa halmashauri zote za wilaya na serikali za mitaa  na kuweka utaratibu wa kupata taarifa kutoka kwa viongozi husika.

Pia, Profesa Mkumbo alitumia fursa hiyo, kuitaka Dawasa kuwalipa madeni wakandarasi wote wanaosimamia miradi iliyokabidhiwa ili miradi hiyo iweze kukamilika na wananchi wakapata huduma hiyo ya maji.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema, wanakwenda kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Profesa Mkumbo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili wananchi wanufaike kwa kunywa maji safi.

Mhandisi Luhemeja aliwaomba wakandarasi kufanya kazi kulingana na mikataba yao inavyowataka kwani Dawasa hawataweza kuvumilia kuona miradi inachelewa kumalizika kwa wakati.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa RUWASA ambaye pia ni, Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu, Enock Wagala alisema, wamekabidhi miradi hiyo kwa Dawasa ila wamekubaliana na serikali kuwa madeni yote zaidi ya Sh. 2 bilioni wanazodai wakandarasi watalipwa ndani ya muda mfupi.

error: Content is protected !!