December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dawasa inavyowatua ndoo kichwani kinamama, JPM atoa neno

Maji ya bomba

Spread the love

MRADI wa maji Kibamba – Kisarawe unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) umezinduliwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)

Mradi huo wenye thamani ya Sh. 10.6 bilioni ukiwa na mtandao wa kilomita 15.65 ulizunguliwa jana Jumapili tarehe 28 Juni 2020 na Rais Magufuli na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi.

Kuzinduliwa kwa mradi huo, kunapunguza adha ya wananchi kutafuta maji umbali mrefu ambapo, Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema, “utaimalisha ndoa kwa kina mama” ambao hatumia muda mwingi kuyatafuta.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Magufuli aliipongeza Dawasa kwa jinsi inavyoshughulika kutatua kero ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

Rais John Magufuli akizindua mradi wa Maji Kisarawe

Pia, Rais Magufuli alipongeza utekelezaji mzuri wa mradi huo, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuwa na mpango mzuri wa upanuzi wa mtandao wa maji.

Rais Magufuli, alitumia fursa hiyo kuitaka menejimenti ya Dawasa kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake. Kauli hiyo iliwafanya wafanyakazi wa Dawasa waliokuwapo kushangilia.

Kiongozi huyo aliipongeza wizara ya Maji kwa utekelezaji wa miradi ya maji nchini ambapo katika kipindi cha miaka mitano miradi 1,423 imetekelezwa nchini kwa gharama ya Sh. 3 trilion.

Alisema kutokana na juhudi hizo za Serikali, hali ya upatikanaji wa maji nchini imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 47 hadi 70.1 (Vijijini) na wastani wa asilimia 74 hadi 84 (Mijini).

Ufanisi wa Dawasa

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo alisema Dawasa kwa sasa ndiyo mamlaka kubwa kuliko zote nchini kutokana na maeneo ya utoaji wa huduma kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kuongezwa.

“Kwa sasa nchi nzima, tuna maunganisho ya wateja wa mamlaka za maji 859,179, kati ya maunganisho haya, maunganisho 310,000 wako Dar es Salaam na Pwani ambayo ni asilimia 35,” alisema Profesa Mkumbo

“Kwa mwezi tunakusanya mapato Sh. 22 bilioni na kati ya fedha hizo, Dawasa inakusanya takribani wastani wa Sh.10 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 45,” alisema

Mtendaji mkuu huyo wa wizara ya maji alisema kati ya maji yanayozalishwa nchi nzima kwa siku lita milioni 835, wastani wa lita milioni 414 zinazalishwa na Dawasa.

Rais John Magufuli akisalimiana na wafanyakazi wa Dawasa

Malengo kufikia 2025

Afisa Mtendaji Mkuu Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema mradi huo wenye mtandao wa kilometa 15.65 za bomba kuu, kilometa 48 za mabomba ya usambazaji, matenki mawili ya lita milioni 6.5 na pampu mbili umejengwa gharama ya Sh. 10.6 bilioni ambapo fedha zote zimetokana na makusanyo ya ndani ya Dawasa.

Mradi huo uliotekelezwa kwa kipindi cha miezi 14 unawanufaisha wananchi wa kata za Kisarawe, Chang’ombe A, Chang’ombe B, Masaki, Kazimzumbani, Masali, Kibuta, Kiluvya, Kwemba, Kisopwa na Mloganzila.

Pia, Dawasa inapanua mradi huo awamu ya pili kwa Sh. 7.3 bilioni kwa kujenga tenki Pugu na mtandao wa kilomita 68 utakaohudumia wananchi wa maeneo ya Pugu, Gongolamboto, Kitunda na Ukonga.

Maeneo mengine ni; Airwing, Banana, Mongolandege, Kinyerezi, Chanika, Mwanagati na Segerea ambapo utaungana na mradi wa maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini.

Luhemeja alisema upatikanaji wa maji kwa jiji la Dar es Salaam wakati Rais Magufuli anaingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015 ilikuwa asilimia 68 lakini kwa sasa imefikia asilimia 88.

“Wakati unaingia madarakani, hali ya maji haikuwa nzuri, Dawasa inazalisha maji lita milioni 300 kwa siku wakati mahitaji yalikuwa milioni 450 na huduma kwa wateja haikuwa nzuri kutokana na mwingiliano mkubwa wa madaraka ambayo kwa sasa yamekwisha,” alisema Luhemeja

“Miaka mitano baadaye, Serikali imefanikiwa kupanua mtambo wa Ruvu Chini kwa kutoa Sh.142 bilioni na kufanya kuongeza uzalishaji wa maji,” alisema

Alisema mwaka 2015 wakati Rais Magufuli anaingia madarakani, maunganisho ya wateja yalikuwa 121,000 lakini kwa sasa yamefikia 310,000.

Luhemeja alisema, mwaka 2015 Dawasa walikuwa wanakusanya Sh.2.9 bilioni kwa mwezi lakini kwa ripoti ya Machi 2020 wanakusanya Sh.12.3 bilioni.

Alisema serikali kupitia Dawasa, imeongeza ajira, mwaka 2015 ilikuwa na watumishi 850, lakini kwa ripoti ya Mei, 2020, inawatumishi 1700 wenye ajira rasmi na 450 za muda mfupi.

Dawasa inatekeleza miradi mingi kwa fedha za ndani ambapo miradi 28 mikubwa yenye thamani ya Sh. 56 bilioni inaendelea kutekelezwa huku miradi 526 yenye thamani ya Sh. 11.4 bilioni.

Luhemeja amesema, kuna mradi wa Mkuranga-Vikindu ulipo zaidi ya asilimia 70 wenye thamani ya Sh. 5 bilioni utakaokwenda kumaliza tatizo la maji eneo hilo pamoja Chalinze kuna mradi unatekelezwa utakaokamilika mwishoni mwa mwaka huu.

“Malengo yetu ifikapo mwaka 2025 tunataka kujihakikishai wananchi wote wa Dar es Salaam na Pwani wanapata maji safi na salama,” alisema Luhemeja.

error: Content is protected !!