October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

David Silinde ajiuzulu

David Silinde, Naibu Waziri TAMISEMI

Spread the love

DAVID Silinde, Mbunge wa Momba, Songwe kupitia Chadema ametangaza kujizulu nafasi ya katibu wa wabunge wa chama hicho kuanzia jana Jumatatu tarehe 4 Mei 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Silinde ametangaza uamuzi huo leo Jumanne tarehe 5 Mei 2020 alipokuwa akizungumza na MwanaHALISI Online iliyotaka kujua uamuzi aliouchukua wa kuhudhuria vikao vya Bunge la Bajeti vinavyoendelea jijini Dodoma kinyume na matakwa ya chama chake.

Mwishoni mwa wiki, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni aliwataka wabunge wote wa Chadema kutohudhuria vikao vya Bunge na kujiweka karantini kwa siku 14 ili kuangalia afya zao kama wana maambukizi ya virufi vya corona au la.

Hata hivyo, wabunge takribani kumi jana Jumatatu akiwamo Silinde walikaidi uamuzi huo wa chama hicho kikuu cha upinzani na kuamua kuhudhuria mkutano wa Bunge ambao ulikuwa ukijadili mapato na makadirio ya bajeti ya wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.

Silinde ambaye amekuwa mbunge kwa miaka kumi mfululizo amesema amechukua hatua hiyo ya kujiuzulu na tayari barua yake ya imemfikia Freema Mbowe.

Amesema, licha ya barua hiyo kumpelekea Mbowe, pia nakala yake ameipeleka kwa John Mnyika, Katibu Mkuu wa chama hicho.

“Nilijiuzulu jana nafasi ya Katibu wa Wabunge wa Chadema, kwa sababu nimeshindwa kusimamia maagizo ya chama ya kutohudhuria bungeni,” amesema Silinde. Hata hivyo, Silinde hajaweka wazi kama atakihama chama hicho au la.

Wabunge wengine walioingia bungeni jana ni; Joseph Selasini (Rombo), Anthony Komu (Moshi Vijijini), Peter Lijualikali (Kilombero), Jafary Michael (Moshi Mjini) na wabunge viti maalumu, Ratifa Chande, Mariam Msabaha na Sabrina Sungura.
Baada ya Silinde kuchukua uamuzi huo, wabunge wa Chadema wamemtaka Mariam Sabaha kujiuzulu nafasi ya Ujumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, kufuatia hatua yake ya kukiuka maagizo ya chama.

Esther Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema, anaunga mkono uamuzi huo wa wabunge wa kumtaka msabaha ajiuzulu.

Mbowe alitangaza uamuzi huo wa wabunge kutohudhuria vikao vya Bunge baada ya kutokea vifo vitatu vya wabunge katika kipindi cha wiki mbili.

Wabunge hao ni; Getrude Lwakatare, Mbunge wa viti Maalumu (CCM), Richard Ndassa, Mbunge wa Sumve (CCM) na Balozi Dk. Augustine Mahiga, aliyekuwa mbunge wa kuteuliwa na waziri wa katiba na sheria.

error: Content is protected !!