May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dar kutoa chanjo ya corona kwa wote

Spread the love

UONGOZI Mkoa wa Dar es Salaam, umeanzisha utaratibu wa kutoa chanjo ya virusi vya corona (UVIKO-19), kwa wananchi wote walio tayari kupata huduma hiyo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na wanahabari leo Alhamisi, tarehe 19 Agosti 2021, Mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla, amesema zoezi hilo litaanza Jumapili, tarehe 22 Agosti mwaka huu, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

“Pamoja kwamba tuna vituo vingi vya kutolea huduma, naelekeza kwamba kuwepo na zoezi la wazi kwa watu wa Dar es Salaam, Jumapili ya tarehe 22 Agosti 2021, katika Uwanja wa Uhuru kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi 10.00 jioni,” amesema Makalla.

Makalla amesema, kama muda uliopangwa kutoa huduma hiyo utaisha pasina wananchi waliojitokeza kupata huduma, zoezi hilo litaendelea hadi wananchi waliofika uwanjani hapo wachanjwe.

“Mpaka saa kumi ikiisha na kama foleni itakuwepo na watu watahitaji chanjo, basi zoezi liendelee mpaka watu watakapoisha,” amesema Makalla.

Amos Makala, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam

Amesema chanjo hiyo itatolewa kwa watu wa rika zote, waliotayari kuchanjwa chanjo ya corona.
Amesema watumishi wa afya zaidi ya 100 wanatarajia kutoa huduma hiyo.

“Zoezi hili tunalianza Jumapili kwa watu wote, baada ya hapo nawalekeza wakuu wa wilaya na wenyewe kutengeneza utaratibu wa eneo kwa siku maalumu, kama wikiendi, mseme wapi katika wilaya zenu mtatoa chanjo,” amesema Makalla.

Aidha, Makalla amewaagiza wakuu wa wilaya za Dar es Salaam, kutenga siku moja ya mapumziko, kwa ajili ya kutoa chanjo hiyo.

Wakati huo huo, Makalla amesema hatosita kuwachukulia hatau watumishi wa afya watakaopangwa kutoa chanjo hiyo, kutoza fedha wananchi.

“Tusitengeze urasimu, chanjo ni bure hivyo msiwatoze wananchi hela,” amesema Makalla.

error: Content is protected !!