January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dangote hafungamani na Prof. Muhongo

Bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote

Spread the love

DOKTA Aliko Dangote, raia wa Nigeria, ni tajiri Na. 1 barani Afrika; wakati Profesa Sospeter Muhongo ni Mtanzania aliyebobea elimu ya miamba (jiolojia).

Wote hao wanapojadili dhana ya uwekezaji kwenye sekta ya uchimbaji gesi asilia na mafuta, wanakubaliana kuwa ni haki kwa wazawa kushiriki katika shughuli hiyo kwa kuwa mchango wao ni muhimu katika kusaidia ukuaji wa uchumi.

Hata hivyo, mitizamo yao kuhusu vipi serikali na wawekezaji wazawa wanaweza kushirikiana katika kutimiza azma hiyo ya kuitumia raslimali hiyo ya gesi na mafuta kwa ajili ya kukuza uchumi wa taifa, inatofautiana.

Dangote: Ni wajibu wa serikali za barani Afrika kuhakikisha kuwa zinawawezesha na kuwapa ushirikiano wawekezaji wazawa ili waingie katika sekta zilizo muhimu za uchumi ikiwemo ya gesi.

Sekta binafsi katika nchi za Afrika ni muhimu katika kuchangia ukuaji wa uchumi na ni vema ikapewa kipaumbele katika miradi muhimu ya kiuchumi ikiwemo madini, miundombinu na raslimali mbalimbali zilizomo barani Afrika.

Prof. Muhongo: Hakuna Mtanzania mwenye uwezo wa kuwekeza katika miradi ya gesi na mafuta, pamoja na wafanyabiashara wenyewe kueleza bayana kuwa uwezo wanao ikiwa serikali itawapa vitalu vya uchimbaji.

“Uwezo wa uwekezaji unaishia kwenye vyombo vya habari, maandazi na juisi. Nataka tu Watanzania waamini wafanyabiashara wa nchini petu wanachoweza kufanya ni kushiriki katika maeneo ya utoaji wa huduma kwa wale wawekezaji wenye mitaji mikubwa wanaowekeza katika shughuli za utafiti na uchimbaji.”

Mtizamo wa Prof. Muhongo unasikitisha na kwa kuwa ndiye waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa sekta ya nishati na madini, amezusha mtafaruku mkubwa na jumuiya ya sekta binafsi.

Anaonekana kama aliyeanzisha jitihada za makusudi kuwanyima wazawa haki ya msingi ya kushiriki katika kumiliki njia kuu ya uchumi kwa kutumia raslimali za ndani ya nchi yao.

Lakini pia, Prof. Muhongo anayejisifu kuwa mwanapinduzi wa uwekezaji katika raslimali hiyo ya gesi na mafuta, amekuwa katika mvutano na wakuu wa jumuiya hiyo hasa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi.

Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, amekuwa akisisitiza serikali ina wajibu mahsusi wa kuwasaidia wafanyabiashara wa nchini kupata uwezo wa kuwekeza kwenye gesi na mafuta.

Siyo tu kwamba msimao wa Prof. Muhongo unatofautiana na ule wa Dk. Dangote, bali hayuko pamoja na mawaziri wenzake Steven Wassira na Dk. Mary Nagu.

Wassira, Mbunge wa Bunda, mkoani Mara, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), anasema: “Lazima watu wabadilike kifikra, watambue kuwa wawekezaji siyo wale tu wanaosubiriwa watoke nje ya nchi kwa kupitia viwanja vya ndege.

Akichangia mjadala wa muswada wa sheria bungeni, uliolenga kuidhinisha sheria ya ubia baina ya sekta ya umma na ya binafsi Sura Na. 103, ya mwaka 2014 (PPP), alisema, “Tunapozungumza uwekezaji tuzungumzie watu wetu. Hawa wawezeshwe ili nao wawekeze na kuiletea nchi maendeleo endelevu.”

Dk. Nagu ambaye ni Waziri wa Nchi anayesimamia Uwekezaji na Uwezeshaji, anasema serikali imeshafanya uamuzi wa kuwajengea nguvu wawekezaji wa ndani ili sekta hiyo ishirikiane na sekta ya umma.

Tanzania ina rasilimali nyingi, lakini hazijafanikiwa kuondoa taifa kwenye umaskini kwa sababu serikali imekuwa ikitegemea tu wawekezaji wageni ambao uzoefu unaonesha sasa mitaji yao inategemea hisia za kisiasa.

“Hatuwezi kutegemea maendeleo kutoka kwa wawekezaji wa nje, kwa sababu wakighairi katika jambo moja, tutashindwa kufikia malengo, hivyo tutateteleka kiuchumi,” anaeleza Dk. Nagu.

Msimamo huu unaendana hasa na mtizamo wa Dk. Dangote ambaye kupitia umoja wa makampuni ya Dangote – Dangote Indutries Group (DIG) – amedhamiria kuiwezesha Afrika kukuza uchumi kupitia mitaji ya ndani.

Huku akitamba kuwa DIG ni kinara wa mabadiliko makubwa ya kiuchumi barani Afrika (Prime movers of Africa Economic Renaissance, anasema jambo la msingi wanaloliona ni kwa serikali Afrika kuwasaidia, kuwawezesha na kuwapa kipaumbele na ushirikiano wawekezaji wazawa ambao wanaweza kuwekeza katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

error: Content is protected !!