July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Daladala walalamikia polisi, Halmashauri Kionondoni

Spread the love

HATUA ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kushindwa kukamilisha ujenzi wa barabara zinazoingia kwenye Vituo vya Daladala Mawasiliano na Makumbusho jijini Dar es Salaam imendelea kulalamikiwa, anaandika Aisha Amran.

Pia malalamiko ya Askari wa Usalama Barabarani kukagua daladala mara kwa mara kwenye vituo hivyo yametiliwa mkazo na watumiaji wa vituo hivyo hususan madereva.

Katika mkutano uliowakutanisha madereva wa daladala na Kikosi cha Usalama Barabarani katika eneo la Kituo cha Mawasiliano, madereva hao wamelalamikia Halmashauri ya Kionondoni na Askari wa Usalama Barabarani kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao.

Abdallah Lubala, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Madereva (TAWDA) amesema kuwa taasisi hizo mbili haziwajibiki ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutofanyia kazi kero zao.

Akizungumza na MwanaHALISI Online baada ya mkutano huo Lubala amesema, umoja huo umekuwa ukiwasilisha kero za ubovu wa barabara za kuingia vituoni lakini pia ukaguzi wa mara kwa mara wa daladala ndani ya vituo lakini hazifanyiwi kazi.

“Kila siku ukaguzi wa daladala ndani ya kituo kwa hakika unaleta usumbufu mkubwa, ni bora wateue siku maalumu ndani ya wiki kwa ajili ya ukaguzi huo,” amesema Daud Msilo ambaye ni miongoni mwa madereva hao.

Akizungumzia barabara amesema, kumekuwepo na kero kubwa kutokana ubovu wa barabara hizo kushindwa kumaliziwa hivyo kuwa chanzo cha kuharibika magari yao.

Pia madereva hao wameeleza kutoridhishwa na namna inavyokabiliana na tatizo la Kituo cha River Side kutokana na baadhi ya madereva kupakia abiria wakiwa barabarani badala ya kuingia kwenye kituo.

Aidha wamekitaka kikosi cha usalama barabarani kanda hiyo kuweka Kituo cha Polisi cha kudumu eneo la River Side au Songas ili kudhibiti magari yanayopakia njiani na kukatisha njia.

Kamanda Zulfa, Mwakilishi wa Mkuu wa Usalama wa Barabarani Kanda ya Kinondoni amesema, wamepokea kero zote na kwamba serikali kupitia Jeshi la Polisi watazifanyia kazi.

error: Content is protected !!