January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dakika 150 kupima wagombea Urais

Spread the love

JUMLA ya dakika 150 sawa na saa mbili na nusu zitatumika kwenye mdahalo wa wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Oktoba 18 mwaka huu. Anaandika Charles William … (endelea).

Mdahalo huo umeandaliwa na taasisi isiyo ya kiserekali ya Twaweza, utafanyika jumapili ya wiki hii ambapo wagombea hao watajieleza ikiwa ni pamoja na kuulizwa maswali.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Twaweza, jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Aidan Eyakuze amesema wagombea wa vyama vitano nchini ndio walioalikwa kwa kuandikiwa barua kushiriki.

Wagombea waliokubali kushiriki pamoja na vyama vyao kwenye mabano ni Anna Mghwira (ACT- Wazalendo), Hashimu Rungwe Spunda (CHAUMMA), John Magufuli (CCM) na Chief Litasola Yemba (ADC) ambapo mgombea wa Chadema, Edward Lowassa bado hajathibitisha kushiriki kutokana na kile kilichoelezwa kuwa na ratiba ngumu ya kampeni.

Eyakuze amesema mdahalo huo utahudhuriwa na wanahabari, wananchi na wadau kutoka asasi mbalimbali za kiraia na kwamba jumla ya wahudhuriaji wanatarajiwa kuwa 1,000.

Pia amesema bado taasisi hiyo inaendelea na mazungumzo na viongozi wa Chadema ili kuweza kufanikisha ushiriki wa Lowassa licha ya kuwa na ratiba ngumu ya kampeni huku wakitoa nafasi kwa mgombea huyo kushiriki kwa kwa njia ya mtandao.

“Mpaka sasa hatujashindwana na viongozi wa UKAWA, sisi kama taasisi tuna ratiba yetu na mgombea wao ana ratiba yake kwa hiyo lazima tufanye mazungumzo ili wafahamu muda, siku, kanuni na mada ya mdahalo. Ni matumaini yetu kuwa watathibitisha katika saa 52 yaliyobaki,” amesema Eyakuze.

Wawawakilishi wa vyama vya siasa vilivyothibitisha kushiriki mdahalo huo wamesema maandalizi ya awali kwa wagombea wao yamekamilika na walio nje ya jiji la Dar es Salaam wanatarajia kurejea Dar es Salaam Jumamosi na Jumapili asubuhi wiki hii.

“Sisi CHAUMMA mgombea wetu yupo fiti na anasubiri tu siku ya tukio tu ili Watanzania waweze kumsikia Rungwe na hatimaye wamuunge mkono,” ameeleza Eugene Kabendera, Katibu Muenezi wa CHAUMMA Taifa.

Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa ADC, Jumanne Magafu amesema wangependa midahalo iwe sehemu ya sheria za uchaguzi ili vyama vyote viweze kushiriki bila kukosa.

Akitoa ufafanuzi juu ya vigezo vilivyotumika kuwaalika wagombea wa vyama vitano kati ya vinane vinavyowania nafasi ya Urais, Eyakuze amesema “vyama vyenye wagombea Urais upande wa pili wa Muungano (Zanzibar) pamoja na vilivyosimamisha wagombea katika majimbo mengi zaidi vilipewa kipaumbele.

Sambamba na wawakilishi wa vyama vya ADC na CHAUMMA, Venance Msebo alikiwakilisha Chama cha ACT – Wazalendo.

Mtayarishaji wa mdahalo huo Maria Sarungi amesema, mdahalo huo utarushwa na kituo cha televisheni cha Star TV saa 7:30 mchana mpaka saa 10:00 jioni na kuwa maandalizi yote yamekamilika.

error: Content is protected !!