July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Cyprian Musiba aingia mitini, wafanyakazi wake kumburuza kortini

Spread the love

 

WAFANYAKAZI wa Kampuni ya CZ Information and Media, wanatarajia kumpeleka mahakamani mmiliki wa kampuni hiyo , Cyprian Musiba, kwa madai ya kutowalipa mishahara miezi mitatu mfululizo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Kampuni hiyo inayomiliki magazeti matatu, Tanzanite, Fahari Yetu na Tanzania Perspective, inadaiwa kutolipa mishahara wafanyakazi wake 68, kuanzia Aprili hadi Juni 2021.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi, tarehe 10 Julai 2021 na Mhariri wa magazeti hayo, Mussa Mkama, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Mkama amesema watafungua kesi katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi (CMA), Jumatatu ya tarehe 12 Julai 2021, ili kudai haki yao.

Mkama amedai kuwa, wamefikia uamuzi huo baada ya Musiba kuingia mitini, tangu Alhamisi ya wiki hii.

“Tuna mdai mishahara ya miezi mitatu, Aprili, Mei na Juni na sasa Julai hiyo inaelekea kwenda kukatika. Juzi Jumatano tumezungumza naye vizuri kwamba, Alhamisi tutakaa kufanya kikao na wafanyakazi tujue mustakabali wetu lakini ametufanyia uhuni,” amedai Mkama.

Mkama amedai “Alhamisi ilifika tumeandaa kikao na wafanyakazi wenzangu, tumempigia simu aje lakini huyu bwana hapatikani, mpaka saa 12.30 jioni hapatikani. Jana Ijumaa tumesema tumtafute tena, hapatikani mpaka muda huu tunapozungumza hapatikani.”

Cyprian Musiba

Mkama amehoji kwa nini Musiba hajawalipa mishahara yao, wakati anajisifu kuwa yeye ni mtetezi wa wanyonge.

“Tunampandisha Musiba mwanaharakati huru mahakani, yeye amejipambanua mwanaharakati wa kutetea Serikali na wanyonge na sisi ni watu wanyonge, sasa anateteaje wanyonge wakati yeye ana wanyonge ndani ya kampuni yake hajawalipa mishahara?” Amehoji Mkama.

MwanaHALISI Online imemtafuta Musiba kwa simu, ili ukupata ufafanuzi wa madai hayo, ambaye amesema “mimi naumwa mzee, nimelazwa huku hali yangu sio nzuri, niko hospitali kitandani. Nikipona nitakwambia.”

Alipoulizwa juu ya madai ya kutopokea simu amejibu “kama wao wameamua kunichafua, ngoja wanichafue. Mimi ngoja nipiganie uhai wangu.”

Kuhusu tuhuma za kutowalipa mishahara wafanyakazi wake miezi mitatu mfululizo, Musiba amedai tuhuma hizo ni njama za maadui wake wanaotaka kumchafua.

“Labda wametumwa tu, si unajua ofisi ina maadui wengi. Labda wametumwa na watu kutaka kunichafua na kunipotezea imani na watu,” amedai Musiba.

Mwanaharakati huyo huru amedai kuwa, wafanyakazi hao hulipwa mishahara kila mwezi.

“Wanapata mishahara kila mwezi hakuna siku hawajalipwa, wamepata mishahara vizuri, niache kwanza napigania uhai wangu, naumwa,” amesema Musiba.

error: Content is protected !!