May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CWT yakoshwa na utendaji wa Rais Samia

Kaimu Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Dinnah Mathamani

Spread the love

 

CHAMA cha walimu Tanzania(CWT) kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na namna inavyowajali watumishi nchini wakiwemo walimu. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Kaimu Rais wa Chama hicho Dinnah Mathamani amesema,katika kipindi cha mwaka mmoja Rais Samia tayari ametatua changamoto nyingi za watumishi wakiwemo walimu ikiwa ni pamoja na kulipa madai ya walimu,kupandisha madaraja,ajira,ujenzi miundombinu ya shule na ahadi ya kuongeza mishara mwaka huu.

Katika eneo la upandishwaji madaraja mwaka wa fedha wa 2021/22, amesema walimu wapatao 127 wamepandishwa madaraja huku walimu 52,000 ambao waliathiriwa na uhakiki wa vyeti nao wakiwa kwenye mpango wa kupandishwa madaraja.

Kuhusu suala la ajira Kaimu Rais huyo amesema,katika kipindi cha mwaka mmoja tayari zaidi ya walimu 27,000 wameajiriwa kwa awamu na wengine 12,000 wanatarajiwa kuajiriwa.

“Hii itaongeza idadi ya walimu na hivyo kuwapunguzia walimu vipindi na kuwawezesha kujiandaa vyema katika kufudisha wanafunzi vizuri,” amesema.

Mathamani amezungumzia kuhusu ujenzi wa miundombinu ya shule ambapo amesema jumla ya madarasa 15,000 yamejengwa nchi nzima.

Rais Samia Suluhu Hassan

Amesema kujengwa kwa vyumba hivyo vya madarasa kumeondoa msongamano wa wanafunzi na hivyo kuwafanya walimu kuongeza tija katika kufundisha suala ambalo lina maslahi mapana kwa wanafunzi na Taifa kwa ujumla.

“Suala hili limekuwa ni la msingi sana kwa Taifa, isipokuwa ombi letu kwa Serikali ni kuangalia tatizo la vyoo na nyumba za walimu kwani kuna baadhi ya maeneo hata nyumba za kupaga hakuna,” amesema Mathamani.

Aidha amesema, CWT kinatambua jitihada zinazofanywa na Serikali katika kutatua tatizo la za walimu nchini ambapo jumla ya sh.55.57 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 809.
“Tunaomba utekelezaji na usimamizi thabiti wa jambo hilo ili liweze kutekelezeka kwa wakati na kupunguza changamoto hiyo,” amesema.

Kuhusu ulipaji wa madai ya walimu kiongozi huyo amesema,wapo baadhi ya walimu waliokuwa na madai sugu lakini Serikali imelipa madai hayo na bado inaendelea kulipa madai hayo ya walimu.

“Tunaiomba Serikali, kwa madai ambayo bado yapo yalipwe kwa wakati ili walimu watulie na shughuli ya kufundisha watoto badala ya kutumia muda mwingi kufiuatilia madai yao,” amesema na kuongeza;

“Pia tumefarijika kwa ahadi ya Rais Samia ya kuongeza mishahara kwa watumishi ambao miongoni mwao ni walimu …,kwa hiyo suala la mishara mipya tunalisubiri kwa hamu maana tunajua lipo katika hatua za utekelezaji.”

Kiongozi huyo pia ametoa pongezi kwa Rais Samia kwa kuagiza watumishi wakiwemo walimu walioondolewa kutokana na vyeti feki kulipwa asilimia 5 ya mshahara wao waliyokuwa wakichangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii sambamba na kuwalipa walikuwa wamebakiza muda kidogo kustaafu.

error: Content is protected !!