January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CWT watoa onyo kali

Spread the love

CHAMA cha Walimu wilayani Magu (CWT), kimesema kuwa kitafanya maandamano ya amani kuanzia Oktoba 14 mwaka huu, endapo Serikali haita walipa fedha zao kiasi cha milioni 430. Anaandika Moses Mseti, Magu … (endelea).

Kauli ya CWT inakuja ikiwa ni hivi karibuni serikali kusema kuwa walimu 60, 322 wanaidai Sh. 29.8 bilioni, baada ya kufanyika uhakiki wa madeni yao yanayoanzia Desemba 2013 hadi Agosti mwaka huu.

Katibu wa CWT, wilaya ya Magu, Coloneli Magembe, akizungumza jana alisema kuwa watafanya maandamano hayo endapo serikali itashindwa kuwalipa kiasi hicho kabla ya Oktoba 14 mwaka huu.

Amesema licha ya kukutana na Mkurugenzi wa Halmashauli ya Magu, Paulo Ntinika, lakini amekuwa akishindwa kutoa majibu ya kina na ya kujitosheleza ni lini watawalipa fedha hizo.

Amesema kutokana na Serikali kushindwa kulipa kiasi hicho, watafanya maandamano hadi katika ofisini kwa mkurugenzi huyo hadi pale mwaafaka utakapopatikana.

“Tutaandamana hadi ofisini kwake na kama itashindikana tutakwenda kuweka kambi nyumbani kwake, tumechoka kudanganywa kama watoto wadogo, mbona wao hawajawahi kulalamika kama hawajalipwa stahiki zao,” alihoji Magembe.

Hata hivyo Magembe amesema kuwa fedha wanazoidai serikali ni za malimbikizo ya mishahara, likizo, fedha za uhamisho na walimu kutokupandishwa madaraja kwa wakati.

“Kama hatutalipwa kuanzia leo (jana) mpaka Oktoba 14, tutaandama hadi ofisini kwake, tutafanya maamzi magumu na kama wameshindwa kutulipa fedha zote watulipe hata milioni 162 ili na familia zetu ziweze kuishi,” amesema.

Mwanahalisi Online ilipomtafuta Mkurugenzi wa Magu, Paulo Ntinika, kujibu madai hayo, simu yake ya mkononi haikupatikana hata pale ilipopatikana haikupokelewa.

error: Content is protected !!