CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimegomea uanzishwaji wa Bodi ya Kitaaluma ya Walimu kwa madai, imelenga kumkandamiza mwalimu. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Akizungumza leo tarehe 13 Aprili 2021, na waandishi wa habari katika Ofisi za CWT, jijini Dodoma, Leah Ulaya ambaye ni rais wa chama hicho amesema, tangu mwaka 2019 walipoalikwa kutoa maoni kwenye Kamati ya Bunge kujadili kuhusu uanzishwaji wa bodi hiyo, walikataa kwa nguvu zote.
Amesema, kwa kuwa mapendekezo yao hayakuzingatiwa na iwapo bodi hiyo itaanzishwa kwa nguvu, CWT itajua nini cha kufanyia ili kubaki katika msimamo wao.
“Mnamo mwaka 2019, CWT kilialikwa kutoa maoni kuhusu uanzishwaji wa bodi hiyo ,kimsingi sisi CWT tuliikataa kwa nguvu zote kwa sababu, baada ya kusoma sheria hiyo, tukajiridhisha pasi na shaka kwamba chombo hiki kililenga kumkandamiza mwalimu badala ya kumsaidia,” ameeleza Ulaya.
Amesema, majukumu yaliyooneshwa kwenye bodi hiyo, yanafanana yale yanayofanywa na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) iliyopo sasa.
Ulaya amesema, jana tarehe 12 Aprili 2021, chama hicho kiliitwa tena na Katibu wa Bunge kukutana na kamati ndogo ya Bunge ya Sheria juu ya kanuni za uendeshaji wa bodi hiyo, ambayo msingi wake ni sheria mama ambayo tayari waliigomea tangu mwanzo.
“Katika kikao cha juzi CWT kiliendelea na msimamo wake wa kutaka chombo hicho kisitishwe na badala yake, TSC iimarishwe kwa sababu gharama za uendeshaji wa bodi hiyo, utategemea pesa za mwalimu za mfukoni kwa ajili ya usajili, leseni na ada ya mwaka ambayo siyo chini ya Sh. 50,000 kwa mwaka.
“Pia kuna gharama za kusikiliza mashauri ya mwalimu na gharama za semina ya kila mwaka, ambayo ni lazima kuhuisha leseni hiyo ambapo bila mwalimu kufanya hivyo, atanyang’anywa leseni na hivyo kupoteza sifa ya Kufundisha,” ameeleza Ulaya.
Ametaja sababu nyingine ya kugomea bodi hiyo ni kupunguza utitiri wa vyombo vinavyomsimamia mwalimu.
Dinah Mathaman, makamu wa rais wa chama hicho amesema, wanachohitaji walimu kwa sasa ni utulivu na siyo kuwaongezea chombo ambacho kinaongeza mzigo kwao.
“Kama tunavyoshuhudia kila mwaka, matokeo na taaluma imeendelea kupanda kutokana na walimu kufanya kazi yao kwa tija, kama ni hizo semina, mwajiri anapaswa aone umuhimu wa kumnoa mwalimu kwa kumpa semina kutokana na bajeti aliyoiandaa kutoka katika ofisi yake, na siyo semina na mafunzo kugharamiwa na mwalimu,” amesema Dinah.
Leave a comment