January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF: ZEC tangazeni matokeo, haturudii uchaguzi

Spread the love

WABUNGE wa Chama Cha Wananchi (CUF) wameitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendelea na mchakato wa kumtangaza mshindi halali wa Urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu. Anaandika Sarafina Lidwino …. (endelea).

Wabunge hao pia wamesema, hawatambui kufutwa kwa matokeo kama ilivyotangazwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha na kwamba hawatashiriki katika uchaguzi utakaorudiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya CUF, Mbunge wa Ole ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CUF, Juma Hamad amesema Zanzibar hakuna vurugu za kisiasa kama inavyodaiwa bali wananchi wamechoshwa na serikali ya CCM wanaitaji watangaziwe rais waliyempigia kura ili maisha yaendelee.

“Sisi kama wabunge wa CUF hatutachoka, tutaendelea kuwapigania wananchi wetu kwa kuitafuta haki yetu ndani na nje ya bunge hadi pale kitakapoeleweka Maalim Seif Shariff Hamad atangazwe mshindi.

“Rais John Magufuli hawezi kuwa rais halali kama Maalim Seif hataapishwa kuwa rais maana waliompigia kura Magufuli ndo wanchi hao hao waliompigia Seif,” amesema Hamad.

Hamad pia ametoa msimamo wa Wabunge wa CUF kwa kile kilichotokea bungeni Novemba 20 mwaka huu wakati wa ufunguzi wa bunge la 11 na kusema kuwa, kilichofanywa na wabunge wa upinzani kuzomea na kutoka ndani ya bunge si kosa wala si utovu wa nidhamu bali katiba ya nchi inaruhusu kugoma unapoona hukutendewa haki.

“Kitendo kile kilikuwa ni cha aibu mbele za wageni lakini tulifanya vile ili kuonyesha msimamo wetu kwa kuwa tulitumia utaratiba wa kuandika barua kwa Spika wa Bunge Job Ndugai kumtaka asimkaribishe Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuwa siyo rahisi halali, lakini ikapuuzwa.

“Ndugai ndio amesababisha aibu ile itokee bungeni baada ya kutosikiliza matakwa yetu na kuamua kuwaleta bungeni watu ambao hawana umuhimu, sisi hatujaaibika kama wengine wanavyosema tulizomea ili kuonyesha msimamo wetu,” amesema Hamad.”

Aidha wabunge hao ambao pia wanaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesema walisikitishwa na kauli iliyotolewa na Rais Magufuli wakati wa ufunguzi wa bunge ambapo aliwaita wabunge wa upinzani wote ni watoto na kwamba kwa mamlaka aliyonayo hakupaswa kuwadharau wabunge waliochaguliwa na wanchi kiasi kile.

error: Content is protected !!