January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF yathibitisha UKAWA

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu

Spread the love

UONGOZI wa juu wa Chama cha Wananchi (CUF) umefanya uamuzi wa kihistoria wa kulisabilia jimbo la Kikwajuni kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) utakapofanyika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Kurugenzi ya Mipango na Uchaguzi ya CUF inayoongozwa na Omar Ali Shehe, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi jimbo la Chake Chake, Pemba, imetangaza rasmi kuwa chama hicho hakitateua mgombea.

Taarifa ya kurugenzi hiyo iliyotolewa jana mjini Zanzibar, ikitokana na maamuzi ya kikao cha Kamati Tendaji ya chama kilichofanyika jijini Dar es Salaam Alhamisi, ilisema CUF haitasimamisha mgombea jimbo hilo ingawa wanachama wake watatu walirudisha fomu kuomba uteuzi ili kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mipango na Uchaguzi imesema wazi kuwa chama hicho kinaliwacha jimbo hilo ili Chadema imsimamishe Naibu Katibu Mkuu wake mpya, Salim Ali Mwalimu kugombea ubunge.

“Tulikuwa na wanachama watatu kila nafasi, sasa walioomba kugombea ubunge tumewaondosha na kuwaweka kapu la kugombea uwakilishi. Maana yake wananchi wa jimbo la Kikwajuni, watapigia kura kuamua nani atakuwa mgombea uwakilishi kati ya wanachama sita tuliowachanganya kufuatia uamuzi wetu huu,” amesema Shehe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia sekta ya fedha na uchumi.

Uamuzi huu unaelezwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa Zanzibar, kama unaostahili kupigiwa mfano kwani kwa upande mwingine, ni uthibitisho wa wazi wa namna CUF kilivyo na moyo mweupe katika ushirikiano wake ndani ya UKAWA.

UKAWA – Umoja wa Katiba ya Wananchi – unaundwa na CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD), ukianzia wakati wa Bunge Maalum la Katiba, ambako vyama hivyo viliamua kuungana kwa lengo la kupambana na mkakati wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuvuruga Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyoandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba.

CUF ina ngome kubwa Kikwajuni, jimbo lililopo kwenye kitovu cha siasa za upinzani kwa miaka ya historia, ingawa haijalitia mkononi unapofanyika uchaguzi tangu 1995.

Miaka yote hiyo, imekuwa ikisimamisha wagombea wenye mvuto, na wanaungwa mkono na wananchi, lakini hili ni moja ya majimbo ambayo matokeo yake yamekuwa yakihojiwa uhalali wake kwa kuwa huwepo ishara nyingi kuwa yamepangwa kwa nia ya kuibeba CCM.

Mara zote ikiwemo uchaguzi wa 2000 ambapo matokeo ya jimbo hili yalifutwa kihujuma na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), wahesabuji kura wamenukuliwa wakisema wagombea wa CUF walishinda kwa kura.

Mkaazi mmoja wa Kikwajuni ambaye ni memba wa CUF, amesema uamuzi wa viongozi wao wanauheshimu kwa kuwa unalenga kuiamarisha mshikamano wa vyama vinne katika kurahisisha kuing’oa CCM madarakani.

Mwandishi hakufanikiwa kumpata Mwalimu, kwani simu haikupokewa kwa muda mrefu. Mwalimu ameingia kwenye siasa chini ya mwaka mmoja sasa, akijiunga na Chadema, na harakaharaka kuteuliwa naibu katibu mkuu baada ya mkutano mkuu wa chama hicho Septemba mwaka jana.

Huyu ni kijana mzaliwa wa Zanzibar, mwandishi wa habari mwandamizi na mtoto wa mwandishi na mtangazaji mashuhuri nchini, Fauzia Ismail ambaye ameingia kwenye shughuli za kutoa ushauri wa kitaalamu wa masuala ya habari kwenye kampuni kubwa za biashara ikiwemo ya Bakhressa.

error: Content is protected !!