August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF yampa ‘heko’ Jaji Mkuu

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimepongeza hatua ya Mohamed Othman Chande, Jaji Mkuu wa Tanzania kuwachukulia hatua mahakimu 11 na maofisa 23 wa mahakama kutokana na makosa ya kinidhamu na kimaadili, anaandika Pendo Omary.

Siku ya jana, Jaji Chande alitangaza kuchukuliwa kwa hatua hizo kwa mahakimu wakazi, mahakimu wafawidhi na mahakimu wa mahakama wa mwanzo.

Kulthumu Mchuchuli, Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CUF amesema, “Tume ya utumishi wa mahakama imefanya kazi nzuri ambayo inapaswa kuwa endelevu ili kuujengea heshima muhimili huo muhimu katika kusimamia na kutoa haki kwa wananchi wote.”

Kulthumu amesema zaidi kuwa, wananchi wamekuwa wakiilalamikia mahakama kwa mambo mengi ikiwemo kuchelewesha kutoa maamuzi ya mashauri mbalimbali kwa wakati na baadhi ya watendaji na mahakimu kujiusisha na vitendo vya rushwa.

“CUF pia tunaipongeza mahakama kwa kushughulikia kwa haraka kesi mbalimbali zinazofunguliwa mahakamani, zikiwemo kesi zinazohusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka jana bila kujali upande upi umeshinda.” Amesema.

Huku akidokeza kuwa, wastani wa umalizaji wa kesi kwa mahakama za ngazi zote nchini kwa kipindi cha Januari mpaka Agosti mwaka huu umekuwa wa asilimia 100.

Hata hivyo chama hicho kimetoa tahadhari kwa serikali katika uanzishaji wa mahakama ya mafisadi na kuitaka mahakama hiyo kutenda haki bila kumuonea mtu yeyote wala kutumika kwa malengo ya kisiasa.

“Tunatambua kuwa uanzishwaji wa mahakama hii unatokana na msukumo wa kisiasa zaidi bila kuzingatia rasilimali watu (uhaba wa majaji) na watendaji wengine katika idara ya mahakama, ndiyo maana tunasisitiza umakini na weledi uzingatiwe,” ameeleza Kulthumu.

 

error: Content is protected !!