July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF yakaribia kupata mrithi wa Prof. Lipumba

Prof. Ibrahim Lipumba

Spread the love

BAADA ya Profesa Ibrahim Lipumba kuchukua uamuzi wa ghafla wa kujiuzulu uenyekiti wa CUF jana, vikao muhimu vya dharura vimeanza kwa lengo la kujaza nafasi hiyo. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Profesa Lipumba ambaye baada ya kuzongwa na Wazee wa Chama asichukue uamuzi huo sasa, jana asubuhi alikimbilia Hoteli ya Peacok, katikati ya jiji la Dar es Salaam, na kutamka kuwa amejiuzulu.

Uamuzi wake ulishtua wengi na kuleta fadhaa na tafrani. Hata hivyo, ufundi wa uongozi uliobaki chini ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, umefanikiwa kurudisha utulivu.

Maalim Seif ambaye alikuwa Dar es Salaam Jumanne na kuondoka jioni Jumatano baada ya kuhudhuria vikao vya mwisho vya kumaliza mgawano wa majimbo ya uchaguzi miongoni mwa vyama vinavyoshirikiana katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), juzi alilazimika kurejea haraka Dar akitokea Zanzibar, ili kuhutubia wanachama wa CUF kwenye Ofisi Kuu za Buguruni.

Akihutubia, alitoa msimamo wa chama kukubaliana na Prof. Lipumba kujiuzulu lakini akasema profesa, akiwakilisha CUF katika vikao na wenyeviti wenza wa UKAWA, alishiriki kikamilifu hatua zote za mpango wa umoja huo kumkaribisha Edward Lowassa kujiunga na Chadema ili apitishwe kuwa mgombea urais anayewakilisha UKAWA.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema profesa huyo ndiye alikuwa mbele katika kumsafisha Lowassa katika tukio lililooneshwa moja kwa moja na televisheni nchini.

“Profesa alikuwa wa kwanza kumsafisha Lowassa… kwa hivyo nasema CUF ipo imara na itazidi kuwa imara ndani ya UKAWA. Tupo na kwa hatua tuliyoifikia, hatuna shaka Magufuli Ikulu ya Kigamboni hataiona kabisa,” amesema.

Akiwa juu ya jukwaa lililioandaliwa haraka ili kukidhi shauku ya wanachama wa CUF waliokusanyika kutwa nzima jana kwenye Ofisi Kuu za chama hicho, baada ya kusikia tamko la Profesa Lipumba, Maalim Seif alisema kufuatia tamko hilo, aliagiza kikao cha Kamati ya Utendaji (Kamati Kuu) kifanyike leo na kufuatiwa na kile cha Baraza Kuu la Uongozi (Halmashauri Kuu).

Mapema Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alikutana na waandishi wa habari mjini Zanzibar, na kutoa taarifa ya maandishi inayosema chama kimeupokea uamuzi wa Profesa Lipumba na kinauheshimu kwa kuwa ni haki yake kikatiba.

Mwandishi wa habari hizi alithibitishiwa jioni hii kuwa kikao cha Kamati ya Utendaji kilikuwa kinaendelea na kazi, na kutarajiwa kupanga ajenda ya Baraza Kuu linalotarajiwa kufanyika kesho Jumamosi.

Tayari baadhi ya majina yanasikika kutajwa katika wanaofikiriwa kuweza kuchukua nafasi ya mwenyekiti wa muda, likiwemo la Mustapha Wandwi, mwanasiasa mkongwe nchini akianzia na harakati za mageuzi mapema 1990.

Wandwi kwa sasa ndiye Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF, ambaye jana alikuwa sehemu ya viongozi waandamizi waliotumika kutuliza hali ya mambo Buguruni kwa kukutana na waandishi wa habari na kutoa msimamo wa kwamba CUF ipo imara na inaendelea na UKAWA.

Wandwi aliingia katika harakati za kuanzisha mageuzi ya kurudisha mfumo wa vyama vingi nchini, baada ya kutumikia Jeshi la Polisi hadi kufikia ngazi ya Kamanda wa Polisi Mkoa. Alijiunga na CUF baada ya kuhama NCCR-Mageuzi kilichokuwa kimedhoofishwa na migogoro ya uongozi wa juu.

Aliteuliwa kuongoza idara ya ulinzi na usalama baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa chama hicho mwishoni mwa mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Moja ya mambo aliyoyalalamikia Profesa Lipumba ni uamuzi wa chama kukubali kumvua uongozi Juma Duni Haji aliyekuwa makamu mwenyekiti, ili ajiunge na Chadema, na kupewa kijiti cha kuwa mgombea mwenza wa kufuatana na Lowassa.

Lowassa alijiunga na Chadema wiki iliyopita baada ya kujiengua Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama alichotoa mchango mkubwa katika kukijenga akiwa miongoni mwa makada wachache waliobaki wa umri wake wanaokijua vizuri kimfumo na itikadi.

Amelalamika kuwa kwa hatua ya kukata jina lake kinyume na kanuni zinazolindwa na Katiba ya CCM, hawezi kuwa mnafiki kusema kuwa bado anaaminika huko.

Lowassa amejiunga chama ambacho kimejipatia sifa kubwa ya kupinga ufisadi serikalini na katika CCM, na kikimtaja kama mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi hata kumjumuisha katika orodha ya mafisadi iliyotangazwa 15 Septemba 2007 na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa.

error: Content is protected !!