CHAMA cha Wananchi (CUF), kimekana kuwatambua wanachama 374 waliotangaza kujivua uanachama, kikidai katika kundi hilo wanachama wake hawazidi 60 na kwamba wengi wao wamekodiwa kwenda kukichafua. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Madai hayo yametolewa leo Ijumaa, tarehe 24 Februari 2023 na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma CUF, Mhandisi Mohamed Ngulangwa, akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu.
“Waliokuwepo eneo husika hawazidi wanachama wetu 60, maana yake ningehesabu ningesema wako 40 au 30 sababu nimefuatilia mkutano wao uliorushwa mubashara (Live) kupitia baadhi ya vyombo vya habari, kuna wakati msema chochote (MC) alisema watu warudishe kadi na idadi ya waliosimama ni wachache sana,” amedai Mhandisi Ngulangwa.
Mhandisi Ngulangwa amedai “tuna ushahidi wako wengine walipewa 5,000 kwa ajili ya kukusanyika hapo ili waonekane wengi lakini kiukweli hakuna wanachama wanaofika 374. Kati ya waliokuwemo kwenye mkutano wengine walionesha kushangazwa kwa kuwa hawakujua kwamba waliitiwa hilo, cha kushangaza wengi, ukumbi ulijazwa na wanachama kadhaa wa Chadema.”
Jana tarehe 24 Februari 2023, wanachama hao wakiongozwa na Shahada Issa, walitangaza kujiondoa CUF huku sababu kuu ya kuchukua uamuzi huo wakidai Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, amekuwa akikiuka katiba, kwa kufanya maamuzi binafsi badala ya kushirikiana na vikao vya chama.
Walidai kuwa, Prof. Lipumba amekuwa akiwafukuza kinyume cha sheria baadhi ya viongozi wa CUF na kuwateua wengine ambao wamewataja kama “mizigo”, huku wakidai kwamba kumekuwa na ubadhirifu wa fedha za chama.
Akijibu tuhuma za Prof. Lipumba kufukuza viongozi kinyemela, Mhandisi Ngulangwa amedai, “mabadiliko ya nafasi ya ukatibu mkuu wanayolalamikia yalifanywa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, baraza lilifanya tathimini ya utendaji wa katibu mkuu na kuona mapungufu na limekuwa likitokea namna ya kufanya marekebisho na maonyo lakini hayakutekelezwa. Mabadiliko hayo hayakufanywa na Prof. Lipumba.”
Kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za chama, Mhandisi Ngulangwa amedai “wote tunafahamu CUF kimepata mbunge mmoja bara na wawili Zanzibar, katika mazingira haya ruzuku ambayo chama inapokea kwa mwezi ni Sh. 8 milioni, hebu taja idadi ya viongozi waliokuwepo, zingatia huduma ya uendeshaji wa taasisi kwa mwezi.”
“Ikiwemo kuwalipa watendaji, gharama za maji, umeme na stationeries. Vyama vinakuwa na huduma nyingi sasa gawa hiyo milioni nane Tanzania Bara na Zanzibar, niambie mtu anawezaje simama hadharani kusema hela inaliwa na wachache?” amedai Mhandisi Ngulangwa.
CUF kimekuwa kikikabiliwa na migogoro ya hapa na pale tangu chama hicho kilipowafukuza baadhi ya wanachama wake katika nyakati tofauti tofauti, ikiwemo waliokuwa viongozi wake saba Novemba 2021, kwa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya chama.
Miongoni mwa viongozi waliofukuzwa ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CUF, Abdul Kambaya, Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF Taifa, Hamis Mohamed Faki na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya chama hicho Taifa (JUVICUF), Hamidu Bobali.
Leave a comment