November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF ya Lipumba yaunda kambi yao ya upinzani bungeni

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kinachomuunga mkono Prof. Ibrahim Lipumba wametangaza kuunda kambi yao Bungeni tofauti na Kambi Rasmi Bungeni inayoundwa na UKAWA, anaandika Dany Tibason.

Imeelezwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha CUF Bara, Magdalena Sakaya ambaye pia ni mbunge wa Kaliyua aliwasilisha majina ya viongozi wapya wa chama hicho kwa Spika wa Bunge Job Ndugai.

Katika majina yaliyowasilihswa kwa Spika wa Bunge ni pamoja na jina la Maftaha Nachuma ambaye ni mbunge wa Mtwara Mjini ambaye amechaguliwa kushika nafasi ya mwenyekiti wa wabunge wa CUF bungeni.

Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliwaambia wabunge
jana bungeni kuwa ofisi ya Spika ilipokea orodha mpya ya viongozi wa CUF Agosti 8, mwaka huu kwa kueleza kuwa chama hicho kinautambua uongozi huo kwa sasa.

Kabla ya mabadiliko hayo Mwenyekiti wa wabunge wa CUF alikuwa mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea ambaye anaunga mkono uongozi wa Maalim Seif na kupinga uongozi wa Prof. Lipumba.

“Mnamo Septemba 8, mwaka huu, ofisi ya Spika imepokea Ripoti kutoka kwa Sakaya na kuonyesha mabadiliko yaliyofanywa na mkutano wa chama hicho Septemba 6, mwaka huu.

“Kulingana na mabadiliko mapya, Nachuma anakuwa mwenyekiti wa wabunge wa CUF na Katibu atakuwa mbunge wa viti maalum, Rukia Kassim Ahmed,” alieleza Dk. Tulia.

Hata hivyo, Mbunge wa Malindi ambaye ndiye mnadhimu kwa chama hicho, Ally Salehe (CF) aliomba mwongozo wa spika akisema kuwa wabunge wa chama hicho wakiwa zaidi 40 walichagua viongozi na kwamba walipoondoka wabunge nane kulibaki nafasi zilizowazi.

Amesema walishafanya uchaguzi wa kujaza nafasi hizo ikiwemo nafasi ya uenyekiti iliyoachwa wazi na Riziki Ngwali ambapo walimchagua Mbunge wa Temeke, Mtolea.

Akahoji ni nani anaamua kuhusu uongozi wa wabunge bungeni ni wabunge wachache ama walio wengi.
Pia alitaka kufahamu kwasababu wao wameshafanya uchaguzi inawezekana kuwa na uongozi juu ya uongozi.

Akijibu Dk. Tulia amesema spika amepokea taarifa ya viongozi hao lakini hajapokea taarifa ya uchaguzi wa upande wakina Ally Salehe.

Amesema watakapoleta taarifa yao ndipo spika ataamua.

error: Content is protected !!