July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF wampinga Prof. Muhongo

Spread the love

JUMUIYA ya Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) imesema wanasikitishwa na uteuzi wa baraza la mawaziri lililotajwa juzi na Rais John Magufuli na kudai  kuwa, katika baraza hilo wamerudishwa wale mawaziri waliokumbwa na kashfa za ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Pia imesema katika baraza hilo hakuna uteuzi  ambao umewiana hasa katika suala la usawa wa kijinsia na wala haukuzingataia Muungano uliokuwepo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini  Dar es Salaam,  Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Hamidu Bobali  amesema  wanashangaa kuwaona  aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Harson Mwakyembe kuwepo tena.

Amesema,  Waziri Muhongo alikuwa anatuhumiwa na suala la Escrow na akajiuzulu halafu Magufuli amemrudisha tena kitu ambacho kinawakosesha amani.

“Inatusikitisha sana kitendo cha Rais wetu kumteua tena Waziri Muhongo kurudi tena wizarani hapo wakati alikuwa na kashfa kubwa ya escrow lakini amerudishwa tena inaonyesha Magufuli pia pamoja na kusifiwa juu ya utendaji wake hayuko makini,”amesema Bobali.

“Pamoja na Muhongo pia Waziri Mwakyembe alikuwa katika wizara ambayo sasa hivi  inakubwa na matatizo makubwa ya kupitisha makontena na wakati  alikuwa waziri   katika wizara hiyo, hilo lilitosha kwa Magufuli kufanya upembuzi wa Mawaziri. Hao wote hawakufaa tena kuridi kuwa mawaziri,” amesema.

Ameongeza kuwa,  wanasikitishwa sana kwani ile kasi ambayo  Magufuli alianza nayo wanaiona inakufa siku si nyingi kwa kuwarudia tena mawaziri hao mizigo.

“Wananchi tunasikitika sana kwa kuwa tulimuamini  Rais Magufuli lakini imani hiyo inakaribia kukatika kutokana na kurudishwa kwa mawaziri hawa na kusababisha kasi kupungua,”ameeleza

Aidha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo hakuwahi kupatikana na hiyo ya Escrow kwani alijiuzulu mwenyewe. Kwa kuhofia kupatikana na hatia.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti huyo alizungumzia mgogoro uliokuwepo Zanzibar na kusema kuwa Baraza la vijana wa chama hicho kwa kushirikiana na vyama vinavyunda Umoja wa Katiba Wananchi (Ukawa) wameandaa mkutano juu ya kuzungumzia mgogoro huo.

“Tunafurahishwa na mazungumzo yanayoendelea kati ya viongozi kwetu wa huko Zanzibar lakini baraza letu limeandaa mkutano huo ili kuzungumzia suala hili,”amesema Bobali

Hata hivyo Bobali amesema wanamuomba Rais Magufuli kuliingilia kati suala la Zanzibar kwani kutokufikia kikomo kunasababisha mambo mengi kurudi nyuma ikiwa moja na uchumi kushuka.

“Jumuiya ya vijana inawatahadharisha wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuacha mara moja kauli chafi na  vitendo vya kichochezi vinavyofanywa na wanachama hao kwani vinaweza kuamsha hasira za vijana wa CUF Zanzibar,” amesema Bobali.

error: Content is protected !!