August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF: Tutaamua na UKAWA

Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF.

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetangaza kwamba katika kushiriki uchaguzi mdogo wa udiwani Bara na ubunge Dimani Zanzibar kitasimamisha wagombea kutegemea na maamuzi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), anaandika Jabir Idrissa.

“… Kwa sababu hizo, CUF inaendelea na mazungumzo na vyama vingine vinavyounda UKAWA kuona namna bora ya kushiriki chaguzi hizi na kuhakikisha kuwa tunaibwaga CCM,” imesema taarifa ya chama hicho.

Taarifa hiyo imetolewa jioni hii kufuatia kikao cha Kamati ya Utendaji ya CUF, chini ya mwenyekiti wake Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho.

Taarifa hiyo imesema utaratibu wa ndani ya chama katika kuwapata wagombea utatekelezwa kama kawaida kupitia ngazi husika za chama, lakini maamuzi ya nani atagombea wapi, yatatolewa baada ya mashauriano na vyama vingine vitatu vinavyounda umoja huo.

Mbali na CUF, Ukawa ni umoja unaoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).

Hivi karibuni, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza ratiba ya uchaguzi mdogo inayohusisha viti 22 vya udiwani Bara na kiti cha ubunge jimbo la Dimani, Wilaya ya Magharibi, Unguja, ambacho kimekuwa wazi baada ya kifo cha Hafidh Ali Tahir aliyekuwa mbunge hapo.

CUF imeshughulikia pia suala la tamko la Mkurugenzi wa Uchaguzi kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima linalosema CUF italazimu kufanya uteuzi wa wagombea kwa utaratibu wa wagombea wake kuidhinishwa na mwenyekiti wa chama na katibu mkuu.

Kailima akitangaza sharti hilo alisema linatokana na mazingira ya chama hicho kuwa katika mgogoro wa uongozi. Ametaja kuwa sharti hilo linatokana na kipengele 4(5)(iii) cha Sheria ya Uchaguzi alichodai kuwa kimewekwa kwa ajili ya chama kilicho katika mvutano na kuwepo pande mbili.

CUF katika taarifa yao hiyo imesema, “Kailima amekitoa wapi kifungu cha Sheria au Kanuni alichokitumia kuweka sharti hilo la ajabu tena kwa chama kimoja tu. Mojawapo ya misingi ya sheria ni kutokuwepo kwa ubaguzi katika utungaji na utekelezaji wa sheria. Huwezi kuwa na sharti linalokihusu chama kimoja tu katika kuthibitisha uteuzi wa wagombea.”

CUF imesema masuala ya kuwapata wagombea wa chama yanaongozwa na Katiba ya chama ya 1992 (Toleo la 2014) na Kanuni za Uchaguzi wa ndani ya chama. Fomu za uteuzi wa wagombea kutoka Tume bya Taifa ya Uchaguzi siku zote huthibitishwa na Katibu wa chama ngazi husika na kwa ubunge na madiwani imekuwa ni Katibu wa Wilaya.

“Kitendo cha Kailima kuja na sharti lake kutoka mfukoni kuihusu CUF katika chaguzi hizi ndogo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu zza uchaguzi na ni muendelezo wa hujuma za dola na taasisi zake dhidi ya CUF kwa kumtumia mtu anayeitwa Ibrahim Lipumba. CUF haitozikubali hujuma hizi na itazilinda na kuzitetea haki zake za kiaktiba na kisheria kikamilifu,” imesema taarifa hiyo.

Kamati ya Utendaji imepongeza wanachama wake wote kwa ujasiri wa kukilinda chama chao kwa “mapenzi na nguvu zao zote dhidi ya njama za wanasiasa muflisi ambao wamekubali kujiuza kwa bei rahisi kutumikia watawala wakidhani wanaweza kukivuruga chama hiki… inawahakikishia Kamati ya Utendaji iko imara na itaendelea kufanya kazi ya kukilinda na kukitumikia chama na wajue kwamba tutashinda mapambano haya.”

Profesa Lipumba ambaye alijiuzulu kwa hiari yake 5 Agosti 2015, aligeuka na kubadili kauli Juni mwaka huu alipoamua kutengua uamuzi wake na kutaka kurejea kitini. Uamuzi huo umezusha mvutano ambao umemfikisha kuvuliwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) Agosti mwaka huu.

Anapigania kujihalalisha katika uamuzi ambao umechangiwa na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi wa kusema anamtambua kama mwenyekiti halali.

Kwa hatua hiyo, Bodi ya Wadhamini ya CUF imefungua shauri Mahakama Kuu kuomba mahakama imtake Msajili aache kuingilia maamuzi ya Chama hicho. Kesi inaendelea mahakamani.

error: Content is protected !!