August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF nao wamvaa Rais Magufuli

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimetoa wito kwa watanzania wote bila kujali itikadi zao kujitokeza kumshauri na kumshinikiza Rais John Magufuli airejeshe nchi katika misingi ya demokrasia na utawala wa sheria, anaadika Pendo Omary.

Miezi kumi tangu kuanza kwa utawala wake, Rais Magufuli amekuwa akilalamikiwa kuiendesha nchi pasipo kuzingatia misingi ya sheria pamoja na utawaa bora huku takwimu zikionesha kushuka kwa uchumi kwa kasi.

“Tatizo hili la Ombwe la uongozi linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka. Taarifa zinaonyesha kuongezeka kwa deni la taifa, kushuka kwa ukuaji wa uchumi kwa asilimia 4 kutoka asilimia 9.5, kushuka kwa ukuaji wa sekta ya ujenzi pamoja na kuporomoka kwa sekta ya usafirishaji.

Deni la taifa limeongezeka kwa asilimia 18 na kufikia trilioni 51, ukosefu wa ajira rasmi, maisha ya wananchi hasa wenye kipato cha chini yamekuwa magumu zaidi mbali,” ameeleza Salim Bimani, Mkurungezi wa Habari wa chama hicho.

Bimani amesema, “utumbuaji wa majipu hauwezi kuwa ni sera ya taifa, lazima uunganishwe katika utendaji wa shughuli za serikali zinazolenga kugusa maisha ya watanzania masikini moja kwa moja.”

Amelalamikia serikali ya Rais Magufuli kutokuwa na dira pamoja na vipaumbele sahihi vya kujenga misingi imara endelevu ya maendeleo ya kiuchumi na kidemokrasia. “Rais Magufuli anabomoa na kuuvuruga uchumi wa nchi,” amesisitiza.

error: Content is protected !!