August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF mambo magumu

Salim Biman, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma wa CUF (mwenye kofia) akizungumza na wapiga kura wa Dimani

Spread the love

HALI ya fedha ni ngumu ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) jambo ambalo linaloongeza changamoto katika kampeni za chama hicho kwenye Jimbo la Dimani visiwani Zanzibar, anaandika Hamis Mguta.

CUF mpaka sasa inaidai serikali ruzuku ya jumla ya Sh. 600 milioni ambazo hawajakabidhiwa kutokana na kuwepo kwa mgogoro wa kiuongozi.

Chama hicho cha upinzani cha tatu kwa ukubwa Tanzania Bara na cha pili kwa Tanzania Visiwani, kilitumbukia kwenye mgogoro mkubwa mwaka jana.

Ni baada ya Prof. Ibrahim Lipumba kuandika barua ya kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho Agosti mwaka 2016 na mwaka jana kuandika barua ya kutengua barua yake ya kujiuzulu.

Hatua hiyo iliibua mgogoro wa kiuongozi baada ya kuibuka kwa pande mbili, mmoja ikipinga kurejea kwake na nyingine kubarika kurejea kwake.

Kwa sasa Prof. Lipumba anatambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kama mwenyekiti wa CUF.
Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF ni miongoni mwa wasiokubaliana na uamuzi wa Prof. Lipumba kurejea kwa kuwa, aliomba kutojiuzulu lakini alifanya hivyo bila kulazimishwa na yoyote.

Mzozo huo umeongeza changamoto katika kutekeleza majukumu ya shughuli za chama hicho ambapo Salim Biman, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma wa chama hicho akisema kwamba, wameanza kuchangishana fedha kutoka katika majimbo 54.

Amesema kuwa, hatua hiyo inachukuliwa kutokana na kuwa na uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Dimani unaotarajiwa kufanyika tarehe 22 Januari mwaka huu.

Mpango uliopo wa chama hicho ili kufikia malengo yake ni kuwa, kila wilaya imepewa jukumu la kukusanya na kuwasilisha Sh. 100,000.

Bimani amesema kuwa, CUF ni chama cha watu na kwamba, wadau wake wapo tayari kuchangia ili kiweze kutimiza malengo yake.

CUF inatarajia kuzindua kampeni zake za ubunge jimboni humo kesho ambapo Maalim Seif ataongoza uzinduzi huo katika kumnadi mgombea wa chama hicho Abdulrazak Khatibu Ramadhani.

Pamoja na kufanyika uchaguzi kwenye jimbo hilo visiwani Zanzibar, pia kutakuwepo na uchaguzi wa madiwani nchini kote ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi.

error: Content is protected !!