January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF:  Kauli ya Jecha haiathiri msimamo wetu  

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema taarifa iliyotolewa jana na Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ya kutotambua uhalali wa kujitoa kwa baadhi ya wagombea katika uchaguzi wa marudio, haitaathiri msimamo wa chama hicho…anaandika Regina Mkonde.

Wakizungumza na MwanaHALISI Online baadhi ya viongozi wa CUF jijini Dar es Salaam leo, wamesema kutoshiriki kwao uchaguzi wa marudio ni halali, wala hawajavunja sheria na katiba kama alivyosema Jecha.

Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Umma wa CUF Taifa, amesema Jecha anajaribu kuudanganya umma kwa kutumia vifungu vya sheria na katiba ambavyo havina uhalisia wa anachokisema.

“Katiba inasema mgombea ana haki ya kugombea na kujitoa katika uchaguzi kama hataki kugombea na si kumlazimisha kugombea kwa masilahi ya kundi fulani,” amesema Kambaya.

“Wagombea wa CUF hawajitoi kwenye uchaguzi sababu uchaguzi walishafanya tarehe 25 Oktoba mwaka jana, ila tume ikatumia ujanja kuufuta na kulazimisha kurudiwa kwa uchaguzi,” amesema Kambaya.

“Uchaguzi wa marudio hatuutambui sababu umekiuka sheria, tume haina mamlaka ya kufuta matokeo ya uchaguzi wote, bali wana mamlaka ya kufuta uchaguzi katika baadhi ya maeneo kama kulikuwa na dosari,” amesema.

Amesema kama kulikuwa na makosa ilitakiwa chama chenye malalamiko kwenda mahakamani kupinga matokeo na si tume kuingilia kati na kuufuta uchaguzi kiholela.

Kambaya amesema CUF haina sababu ya kwenda mahakamani kuapa kutoshiriki uchaguzi kwani hawakujaza fomu ya kushiriki uchaguzi wa tarehe 20 Machi, bali walijaza fomu ya kushiriki uchaguzi wa 25 Oktoba mwaka jana.

Shaweji Mketo, Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, ameuita uchaguzi wa marudio kuwa unafanana na uchaguzi wa maruhani uliofanyika mwaka 2002 kisiwani Pemba ambako wagombea wa CUF walienguliwa kimkakati na wanachama wakaendelea kuwapigia kura dhidi ya wagombea wa vyama vingine.

“Uchaguzi wa marudio utakuwa wa maruhani, wananchi wengi watapiga kura za hapana badala ya ndiyo kama ilivyotokea kwenye uchaguzi wa mwaka 2002,” amesema na kuongeza.

“Nchi yetu huruhusu mgombea kushinda hata kama anakura ndogo za kukubalika kushinda na kuwa na kura nyingi za kukataliwa,”

“Ulifanyika uhuni katika ufutwaji wa matokeo, hebu fikiria tarehe 25 uchaguzi ulifanyika, 27 ilikuwa siku ya mwisho ya kutangaza matokeo lakini Jecha hakuonekana,” amesema.

Mketo ameongeza “Tarehe 28 Jecha alitangaza kufutwa kwa uchaguzi bila ya kushirikisha makamishina wa tume sababu makamishina walikuwa kwenye kikako kumalizia hatua za utangazaji, huku Jecha akioneshwa akifuta uchaguzi katika kituo cha televisheni ya ZBC.”

Mketo amesema, kuna fomu ilikosekana, makamo mwenyekiti alipiga simu kwenye ofisi za tume na kutaka mtu alete fomu, alipoileta alizuiliwa na jeshi, hatimaye makamo huyo kukamatwa na jeshi hilo.

“Chama kinapoweka mgombea lazima kithibitishe kwamba mgombea huyo anatoka chama chao,kujitoa kwa mgombea ni haki yake hazuiliwi na mtu yeyote,” amesema Mketo.

Chama cha CUF kimesema, kwa sasa hakitatoa tamko lolote, kinasubiri hadi mwisho wa uchaguzi wa marudio, kasha kitathmini na kutoa tamko lake.

Jecha alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari jana katika mkutano alioufanya visiwani Zanzibar, akisema kuwa, hadi sasa hakuna vyama vya siasa vilivyofuata utaratibu wa kujitoa katika uchaguzi wa marudio na kwamba tume inawatambua kama wagombea.

“Sisi tunasikia nje kwamba kuna baadhi ya vyama havitashiriki katika uchaguzi wa marudio, lakini hakuna hata kimoja kilichofuata utaratibu wa kisheria na katiba wa kujitoa,” alinukuliwa Jecha.

Jecha aliendelea kusema “ Hawakufuata taratibu za katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kama wengekuwa wamefuata katiba, wangekuwa wametekeleza masharti ya vifungu 31- hadi37A.”

Kwa mujibu wa kauli ya Jecha, vyama vyote vilivyojitoa, majina ya wagombea wake wataendelea kuwepo kwenye karatasi za tume.

Pia, alisema, vyama ambavyo vimekubali kushiriki katika uchaguzi wa marudio ambavyo ni ACT, ADC, CCK, AFP, SAU, TLP na CCM, Tume inawapa ulinzi wa kutosha.

error: Content is protected !!