January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF: Hatutoshiriki sherehe za Mapinduzi

Spread the love

VIONGOZI wakuu wa Chama cha Wananchi (CUF) hawatashiriki shughuli za kiserikali zilizopangwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kutokana na serikali iliyopo kutokuwa na ridhaa ya Wazanzibari. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano na Umma ya chama hicho imesema hatua hiyo inatekelezwa katika kuzuia raslimali za wananchi kutumika vibaya ikiwemo kuendekeza uongozi wa serikali usiohalalika kisheria na kikatiba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kupitia vyombo vya habari, hata Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa CUF na mwanasiasa aliyegombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, ambao ulihujumiwa kwa makusudi, hatahudhuria sherehe hizo zitakazofikia kilele Januari 12, kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Zanzibar.

Taarifa imesema chama hicho kimekuwa kikishiriki sherehe za Mapinduzi tangu kilipoanzishwa kwa kuwa kinatambua umuhimu wa siku hiyo ambayo ilikuwa ndio imeipatia Zanzibar jamhuri chini ya kiongozi wake wa kwanza, Mzee Abeid Amani Karume.

Lakini, taarifa imeeleza, malengo ya Mapinduzi hayo yalikuwa ni pamoja na Zanzibar kupata uongozi wenye ridhaa ya wananchi, na sio kama ilivyo sasa serikali kuwa iliyojiweka baada ya maamuzi ya wananchi kuhujumiwa.

Kuhusu asili ya Mapinduzi, imeelezwa kuwa CUF inatambua Mapinduzi ya 12 Januari, 1964 yanahusu Wazanzibari wote na malengo yake makuu kuelezwa na kufafanuliwa vyema kupitia Dikrii Na. 6 ya mwaka 1964 iliyopitishwa na Baraza la Mapinduzi.

Katika Dikrii hiyo, malengo yanatajwa kwamba ni kuleta usawa, umoja na maridhiano baina ya Wazanzibari wote na kupiga vita aina zote za ubaguzi.

Taarifa imesema kwa kuwa tayari umma wa Wazanzibari umetangaziwa kwamba kuanzia Januari 2 kutakuwa na s hughuli mbalimbali zinazolenga maadhimishio ya Mapinduzi na hatimaye kama ilivyo desturi, kilele chake kufikiwa Januari 12, 2016 kwenye Uwanja wa Amaan, “viongozi wa CUF hawatoshiriki ratiba walizopangiwa mpaka pale chaguo la wananchi wa Zanzibar walilolifanya tarehe 25 Oktoba, 2015 litakapoheshimiwa.”

CUF inasikitisha sherehe za mara hii zinafanyika wakati nchi na watu wake wema wapo katika mtihani mkubwa kufuatia kitendo cha mtu mmoja, Jecha Salim Jecha, kuamua kwa utashi wake na waliomtuma, kuiingiza nchi katika msukosuko na taharuki kwa kudai eti ameufuta uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na matokeo yake.

“… Amevunja Katiba, amevunja Sheria ya Uchaguzi na amevunja hata maadili ya kazi yake, (hivyo) mara hii nchi yetu itaadhimisha Mapinduzi huku Serikali ikiwa inaongozwa na viongozi wasiokuwa na uhalali na ridhaa ya wananchi,” imesema taarifa ya CUF iliyosainiwa na Mansour Yussuf Himid, Mshauri wa Katibu Mkuu wa chama.

Taarifa imesema kwamba ni msimamo wa CUF tangu hapo kuwa hakikubaliani na uamuzi huo wa mtu mmoja kujinyakulia mamlaka ya wananchi wa Zanzibar yaliyowekwa kikatiba, na kwa msingi huohuo, “tunapenda kutumia fursa hii kuwaeleza wananchi wa Zanzibar kwamba viongozi wetu hawatoshiriki katika shughuli walizopangiwa katika ratiba ya sherehe hizi.”

Chama kimetoa sababu nne za kufikia uamuzi huo wa viongozi wake kutoshiriki sherehe za mwaka 2016. Sababu hizo ni zifuatazo:

  • Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 (Toleo la 2010), Ibara ya 28, Ibara ya 42(2), Ibara ya 48(b), Ibara ya 90(1) na Ibara ya 92(1) Serikali iliyokuwepo madarakani na Baraza la Wawakilishi lililokuwepo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010 – 2015) vilimaliza muda wake wa uongozi tarehe 2 Novemba, 2015 kwa upande wa Serikali na tarehe 12 Novemba, 2015 kwa upande wa Baraza la Wawakilishi. Kwa sasa, hatuna viongozi wenye uhalali wa kikatiba kuweza kutekeleza majukumu ya kiserikali. Kwa hivyo, kushiriki katika ratiba hizo kwa kutumia nafasi ambazo hazina uhalali tena wa kikatiba ni kwenda kinyume na dhamira ya waasisi wa Mapinduzi, jambo ambalo hatuko tayari kulifanya.
  • Kiutaratibu, kilele cha sherehe huongozwa na Rais ambaye yupo kikatiba. Kwa mara ya kwanza tokea tarehe 12 Januari 1964, sherehe za miaka 52 zitaongozwa na Rais ambaye ameshamaliza muda wake wa uongozi kikatiba na ambaye hana uhalali na ridhaa ya wananchi wa Zanzibar. Kushiriki katika sherehe hizo ni kuhalalisha kipindi cha uongozi ambacho hakipo tena kikatiba. Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wenziwe ndani ya Chama waliokuweko Serikalini hadi tarehe 2 Novemba, 2015 hawako tayari kuhalalisha uvunjaji wa Katiba ya Zanzibar ambayo ndiyo sheria kuu ya nchi.
  • Viongozi wa CUF wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad wanaamini katika msingi mkuu wa Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 chini ya uongozi wa Baba wa Taifa la Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, ambao ni kuleta utawala wenye ridhaa ya wananchi walio wengi. Msingi huo umewekwa wazi na kutiliwa nguvu na Katiba ya Zanzibar ya 1984 (Toleo la 2010) kupitia Ibara ya 9(2)(a) ambapo inaelezwa kwamba, “Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa Serikali kufuatana na Katiba utatoka kwa wananchi wenyewe.” Mamlaka hayo ya wananchi yalitekelezwa tarehe 25 Oktoba, 2015 kwa kuwachagua viongozi watakaoongoza Serikali yao kwa miaka mitano ijayo. Kitendo chochote cha kupindua mamlaka hayo ya wananchi ni kwenda kinyume na misingi ya Mapinduzi na misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa la Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume. CUF hatuko tayari kushiriki katika kuisaliti misingi hiyo na kuisaliti dhamira ya Mzee Karume.
  • Sherehe za kuadhimisha Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 zina lengo la kukumbuka malengo ya Mapinduzi hayo na dhamira ya waasisi wake wakiongozwa na Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume katika kusimamia utawala wenye ridhaa ya wananchi walio wengi. Kuzitumia sherehe za Mapinduzi kuhalalisha utawala usio na ridhaa ya wananchi wa Zanzibar na ambao haupo kikatiba ni usaliti mkubwa wa dhamira ya kuwepo kumbukumbu hiyo. CUF hatuko tayari kuwa sehemu ya usaliti huo.

CUF inafanya uamuzi huo wakati mgombea wake anayepigania haki ya kukabidhiwa mamlaka kutokana na ushindi alioupata, Maalim Seif, amekuwa akikutana kwa faragha na viongozi wa kitaifa wa Zanzibar akiwemo Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye anashikilia uongozi wa serikali inayopingwa uhalali wake.

Viongozi wengine wanaokutana ni marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Dk. Salmin Amour Juma na Dk. Amani Abeid Karume, pamoja na Balozi Seif Ali Iddi.

Pamoja na vikao hivyo vilivyofikia tisa, hakuna taarifa inayotolewa kwa umma na haijulikani ni lini vitakwisha. Hivi karibuni, Dk. Shein alipokuwa akieleza mazungumzo yake na Rais Dk. John Magufuli wa Tanzania, alisema mazungumzo yatakapomalizika umma utajulishwa matokeo.

Oktoba 28, Jecha alitangaza kufuta uchaguzi mzima kwa madai ya kuwepo matatizo yaliyoutia doa, wakati huo akiwa ameshatangaza zaidi ya asilimia 70 ya kura za urais ikiwa ni majimbo 33 kati ya 54.

Viongozi wa CCM wamekuwa wakishikilia kuwa kutafanyika uchaguzi wa marudio, wakirejea tamko la Jecha alipotangaza kufuta uchaguzi. Tume ya Uchaguzi Zanzibar haijatangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio huku kipindi cha siku 90 kilichotajwa kikiwa kinamalizika.

error: Content is protected !!