CHIEF Lutalosa Yemba, amejitosa katika mbio za urais wa Tanzania, kupitia Chama cha Wananchi (CUF) huku wanachama watano wa chama hicho, wakijitokeza upande wa Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi tarehe 27 Juni 2020 na Mhandisi Mohammed Ngulangwa, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF wakati akizungumza na MwanaHALISI ONLINE kuhusu mchakato wa chama hicho kupata wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.
Chief Yemba aliyekuwa Mgombea Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kupitia Chama cha Alliance Democratic Change (ADC), alirudi CUF mwanzoni mwa 2020.
Katika uchaguzi huo, Chief Yemba alipata kura 66,049 sawa na asilimia 0.43 ya kura zote zilizopigwa milioni 15.19. Mshindi kwenye uchaguzi huo alikuwa Dk. John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura milioni 8.88 sawa na asilimia 58.46.
Mhandisi Ngulangwa amewataja wanachama waliojitosa kugombea urais wa Zanzibar kupitia CUF ni, Abbas Juma Mhunzi, Makamu Mwenyekiti CUF Zanzibar. Faki Suleiman Khatibu, Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar.
Wengine ni, Mhandisi Mohamed Habib Mnyaa, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Mussa Haji Kombo na Rajab Mbarouk.

Mhandisi Ngulangwa amesema, makada hao wa CUF wameshachukua na kurudisha fomu hizo, tangu zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu lilipofunguliwa mwanzoni mwa mwezi Juni 2020.
Aidha, Mhandisi Ngulangwa amesema zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu za kugombea urais, litafungwa katikati ya Julai 2020.
Kuhusu mchakato wa kupata wagombea ubunge, udiwani na uwakilishi, Mhandisi Ngulangwa amesema, tangu mchakato huo uanze, wanachama wengi wamejitokeza kuchukua na kurejesha fomu.
Mhandisi Ngulangwa amesema, mchakato huo utakamilika tarehe 2 Julai 2020.
“Mchakato wa uchukuaji fomu na hatimaye urejeshaji katika nafasi ya udiwani kwa kata za Bara, udiwani kwa wadi Zanzibar, ubunge na uwakilishi na nafasi ya urais wa Tanzania na Zanzibar, tulianza mwanzoni mwa mwezi Juni, na linaelekea ukingoni,” amesema Mhandisi Ngulangwa na kuongeza:
“Tarehe ya mwisho ya kuchukua na kurudisha fomu kwa upande wa wabunge, madiwani na wawakilishi ni tarehe 2 Julai 2020, lakini itaendelea kidogo mpaka kati kati ya mwezi Julai kwa upande wa urais.
Leave a comment