April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

CUF chaibuka na waraka mpya wa elimu

Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeitaka serikali kuufuta Waraka Mpya wa Elimu Na. 4 wa mwaka 2020, kwa maelezo kwamba, utekelezwaji wake utapelekea walimu kushindwa kuwaanda vyema wanafunzi, kwa ajili ya mitihani yao ya kuhitimu masomo. Anaripoti Martin Kamote, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 7 Februari 2020 na Mhandisi Mohamed Ngulangwa, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma CUF.

“CUF kinatoa wito kwa serikali kuufuta au kusimamisha utekelezaji wake, kwa kuwa una hasara nyingi kuliko faida. CUF kinaamini kinachostahili kufanyika awali ni maboresho ya mitaala kabla ya utekelezaji wa marufuku iliyomo ndani ya waraka tajwa hapo juu,” inaeleza taarifa ya Mhandisi Ngulangwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mhandisi Ngulangwa, waraka huo unapiga marufuku ratiba za masomo ya ziada, ratiba za masomo ya mwisho wa wiki na vipindi vya likizo, kitendo kitakacho athiri zaidi shule za kutwa za serikali na binafsi.

“CUF kimeupitia waraka huo, kimsingi umeelekeza kwamba muda wa masomo ya darasani ni kuanzia saa 1:30  asubuhi hadi saa 9:30 mchana, waraka umepiga marufuku  ratiba za nje ya muda huo, ratiba za mwisho wa wiki na wakati wa likizo hata kwa madarasa ya mitihani ya kitaifa,” inaeleza taarifa ya Mhandisi Ngulangwa.

Mhandisi Ngulangwa amesema CUF kimebaini kwamba , waraka huo una mapungufu makubwa yenye hasara nyingi kuliko faida.

“Kwanza mitaala yetu ya elimu ni mirefu kuliko muda  halisi wa kukamilisha mitaala hiyo. Na ni shule chache sana zinazokamilisha mitaala hata kwa kutumia huo muda wa ziada uliopigwa marufuku. Pili masomo kwa vitendo kwa masomo ya sayansi yanahitaji muda mrefu sana na haiwezekani kutumia muda wa kawaida wa darasani,” amesema  Mhandisi Ngulangwa.

error: Content is protected !!