July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF, CHADEMA walia Katiba Mpya kutotengewa fungu bajeti 2022/203

Spread the love

VYAMA vya CUF na Chadema vimesema Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, haiungi mkono malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan kukuza uchumi unaoongeza ajira na kuboresha demokrasia nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo tarehe 19 Juni, 2022 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wameeleza kusikitishwa na hotuba hiyo ya bajeti ya mwaka 2022/2023 kutotenga fungu kwa ajili ya Katiba Mpya.

Prof. Lipumba ambaye ni msomi wa masuala ya uchumi, amesema licha ya Rais Samia kuahidi kuanza ujenzi wa demokrasia, katika hotuba ya bajeti ya bajeti iliyowasilishwa bungeni hakuna fungu la kutekeleza mambo yanayohusu ujenzi wa demokrasia kama kupata tume huru ya uchaguzi na kukamilisha taratibu za kupata katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi.

Amesema mambo hayo hayakuguswa kabisa licha ya kwamba walipokutana na Rais Samia jijini Dodoma katika mkutano wa wadau wa siasa, walikubaliana kwamba Januari mwaka huu kikosi kazi kiwasilishe mapendekezo serikali ili yaanze kufanyiwa kazi ikiwamo kutenga bajeti.

Amesema badala ya kikosi kazi kukamilisha kazi hiyo Januari mwaka huu, sasa kimehamishiwa kwa Rais na muda unazidi kwenda.

“Sijakataa tamaa, nasikitika bajeti hii haiakisi haya mambo, ndio maana tunaendelea na mapambano,” amesema.

Wakati Lipumba akisema hayo, kwa upande wake John Mnyika naye amesema katika uchambuzi wao wa bajeti, wamegundua kuwa rai kubwa ya wananchi ambayo inahusu katiba mpya haijatengewa fedha.

Amesema Serikali haijatenga fedha kwa ajili ya kukwamua, kukamilisha au kuanza mchakato wa katiba mpya.

“Kwa kutokuwepo na fungu au vifungu kuhusu mchakato wa katiba mpya katika bajeti ya serikali, maana yake ni kwamba kuanzia Julai Mosi, 2022 hadi Juni 30, 2023 hautakuwa na hatua za maana za kuufufua na kukamilisha mchakato wa katiba mpya.

“Mradi wa kuhuisha katiba mpya, unapaswa kuingizwa katika bajeti ya serikali kama mradi wa kipaumbele… mradi huu taifa lilishauanza miaka mingi hapo nyuma. Mradi huu ulikwama mwaka 2014 wakati nchi imeshatumia mabilioni ya fedha,” amesema.

error: Content is protected !!