Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CUF: Bajeti ya Serikali ni hewa
Habari za SiasaTangulizi

CUF: Bajeti ya Serikali ni hewa

Spread the love

CHAMA cha Wananchi CUF kimechambua bajeti ya serikali ya mwaka 2018/19 kuwa ni bajeti hiyo ni hewa na haina muafaka kwenye kuinua uchumi wa nchi. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari Julias Mtatiro Mwenyekiti kamati ya uongozi ya chama hicho leo Juni 24 2018 kwenye ofisi za wabunge wa chama hicho magomeni jijini Dar es Salaam

Mtatiro amesema kuwa bajeti hiyo haikuangaza kwenye sekta kilimo ambayo ndio sekta muhimu katika kiunua uchumi wa nchi ambapo sekta hiyo imewepa bajeti ya Bilioni 170.27 ambapo ni asimia 0.25 ikilinganisha na sekka nyengine.

“Ni aibu kuona bajeti nzima haifiki hata asilimia mbili kwenye sekta ya kilimo …hii ndio sababu ya nchi yetu kutokuwa na maendeleo ya kiuchumi,” amesema Mtatiro.

Amesema kuwa asimilia 70 ya watanzania uchumi wao unategemea kilimo hivyo serikali isikwepe kuinua sekta hiyo na kwamba sekta hiyo ndiuo inaweza kunyanyua uchumi wa nchi kama ilivyokuwa kwa nchi ya Singapol.

Chama hicho kimeweka wazi kuwa kitaruhusu maandamano kwa wabunge na wananchi wa mikoa ya kusini kushinikiza kutoa asimia 65 za maozo ya korosho ya nje kabla ya tarehe 30 Juni mwaka huu.

Soma zaidi mapendekezo ya Chama hicho

MAPENDEKEZO YA JUMLA YA THE CIVIC UNITED FRONT [CUF-CHAMA CHA WANANCHI] KUHUSU BAJETI KUU YA 2018/19

MAELEZO YA MWENYEKITI WA KAMATI YA UONGOZI TAIFA MHE. JULIUS MTATIRO MBELE YA WAANDISHI WA HABARI [PRESS CONFERENCE] ILITOFANYIKA LEO JUMAPILI TAREHE 24 JUNI, 2018 KATIKA OFISI YA WABUNGE WA CUF MAGOMENI-DAR ES SALAAM.

Ndugu wanahabari,

Leo tumewaiteni hapa ili kuwashirikisha mtizamo wa The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2018/19, jambo ambalo ni la muhimu sana kwa wakati huu.

UTANGULIZI

Katika mwaka wa Fedha 2018/19, Serikali ya Awamu ya Tano imewasilisha Bungeni Bajeti ya Taifa ambayo inafikia Shilingi za Kitanzania 32.4 trilioni.

The Civic United Front (CUF), kama mdau muhimu wa uchumi wa nchi yetu, tumeona kuwa yako masuala ambayo tunapaswa kuishauri serikali wakati huu na wakati wa utekelezaji wa bajeti hiyo.

Uchambuzi wetu utagusa maeneo makuu matano; Sekta maalum za kukuza uchumi jumuishi, Masuala mtambuka, Kutotekelezeka kwa bajeti iliyopita, Bajeti hewa ya 2018/19 na Mapendekezo ya jumla;

1) The Civic United Front (CUF) kinaona kwamba, kama serikali ya CCM ambayo ina dhamana ya uongozi wa nchi haitabadilika na kuanza kupendekeza na kutekeleza bajeti halisi za nchi, tutaingia kwenye matatizo makubwa sana. Hali hiyo inatufanya tuishi katikati ya “uongo wetu sisi wenyewe”kwa muda mrefu, matokeo yake sote huanza kuona uongo huo ni ukweli kumbe tunaliua taifa letu.

CCM imekuwa inaongoza nchi kama SACCOS binafsi, hakuna mwendelezo wala uwiano wa mipango, bajeti na utekelezaji kutoka utawala mmoja kwenda nyingine au kutoka mwaka mmoja kwenda mwaka mwingine katika utawala uliopo.

Ndiyo maana serikali iliyomaliza muda wake mwaka 2015 chini ya JK na Pinda wa CCM iliwaaminisha watanzania kuwa kipaumbele cha taifa ni Kilimo Kwanza (hewa). Ghafla amekuja JPM kipaumbele cha taifa ni viwanda, kuhamia Dodoma, kununua ndege, kujenga viwanja vya ndege n.k. Tutakuwa taifa la hovyo sana kama tutaendelea na michezo hii.

2) Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa taifa la Tanzania, na serikali yoyote ile ambayo haitawekeza walau asilimia 20 ya bajeti yake kwenye sekta hii, serikali hiyo itamaliza muda wake na kuliacha taifa likiwa ni masikini kupita kiasi.

Kanuni za juma za uchumi zinayataka mataifa kuwekeza kwenye sekta ambazo zinaajiri na kutegemewa na watu wengi zaidi kuliko zile ambazo hazina muunganiko wa moja kwa moja na wananchi.

Tanzania haitainuka kamwe kama haitawekeza kwenye kilimo, Tanzania haitatatua tatizo la ajira kama haiwekezi kwenye kilimo, hatutaongeza mapato ya uhakika kwenye taifa bila kilimo, hatutajenga viwanda bila kilimo cha uhakika.

Utaratibu huu wa kutenga chini ya asilimia 2 ya bajeti ya taifa letu kuinua kilimo, ni tiketi ya kututokomeza kwenye tope zito la umasikini.

3) Serikali ikomeshe mara moja utaratibu wa “double standard” katika kutekeleza bajeti zinazoidhinishwa na bunge, utaratibu huo ni wa hovyo na si wa kiungwana, unaua morali na utendaji wa sekta za serikali.

Katika bajeti ya 2017/18 kuna wizara na idara zimepewa bajeti za zaidi ya asilimia 300 kuliko ilivyoidhinishwa na bunge huku zingine zikinyengwa na kupewa chini ya asilimia 10 tofauti na ilivyoidhinishwa na bunge.

Bunge litimize wajibu wake. Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) imeonesha kuwa serikali inatekeleza masuala mengi mno kinyume kabisa na bajeti iliyoidhinishwa na bunge. Kwa hiyo hivi sasa tuna bajeti ya bunge na bajeti ya serikali hata baada ya bunge kupitisha bajeti moja.

Mtindo huu ni mfano wa wazi wa namna serikali inavyojiamulia mambo makubwa ya kiuchumi na kulipiga bunge kikumbo bila kujali kuwa bunge ndilo chomo cha mwisho cha uidhinishaji na usimamizi wa utekelezaji wa bajeti. Tutajengaje taifa linalosimamia na kutekeleza bajeti zake kwa uzito, nidhamu na uhalisia ikiwa bunge linadharauliwa kiasi hiki na halina cha kufanya?

4) Serikali rukaruka, itulie iache mtindo wa kutokuwa na mwelekeo unaojulikana. Serikali ikomeshe tabia yake ya kuanza miradi na kuitelekeza na kurukia mingine. Mfano kulikuwa na mradi wa gesi inayotokea Mtwara na miaka michache iliyopita taifa zima liliaminishwa kuwa kupitia mradi huo tatizo la umeme litakomeshwa nchini.

Hivi sasa serikali hiyo hiyo, chama kile kile na viongozi wale wale wanaanza kuuaminisha umma imani mpya ya kwamba suluhisho la umeme ni mradi wa Stiegler’s Gorge na imekimbilia huko. Hatuwezi kwenda mbele kwa kurukaruka namna hii.

5) Serikali ifikirie mara mbilimbili kabla ya kutekeleza mfumo wa fedha wa “Treasury Single account (Akaunti Kuu ya Hazina)” ambapo fedha zote za serikali zitakuwa zinaingizwa kwenye akaunti moja peke yake. Kwa mtizamo wa chama chetu athari za mfumo ni pale ambapo serikali itajipa mamlaka makubwa zaidi ya kuweka urasimu au kutotoa kabisa fedha hizi na kuzirudisha kwenye maeneo ambako zinapaswa kurejeshwa kwa wakati.

Mfumo huu unaopigiwa chapuo na serikali ili ni jambo la hatari zaidi, ni kama vile tunaua “D by D”, tunaua Serikali za Mitaa, tunaua Mashirika muhimu ya serikali na tuanawaua wananchi wa kawaida. Kwa kama ya kwetu, ni muhimiu serikali ikajenga mfumo wa kutambua fedha zilizomo kwenye akaunti ya idara zake, mashirika yake na halmashauri zake kila siku, kuliko kuchukua makusanyo yote.

i. Serikali za Mitaa kwa maana ya Mamlaka za Halmashauri za Wilaya, zinakufa, ziko ICU. Serikali ichukue hatua za makusudi na kusahihisha makosa yake na mkakati wake wa kuzipora Serikali za Mitaa uwezo wa kiuchumi na kutaka serikali hizo zifanye kazi kutokea serikali kuu.

Mwalimu Nyerere mwenyewe aliua Serikali za mitaa baadaye akatambua makosa yake akazirejesha, ukiua Serikali za Mitaa umeua moyo wa nchi, nchi zote ambazo zimeendelea kwa uhakika hapa duniani, zimefanya hivyo kwa mchango mkubwa sana wa serikali za mita.

Nchi hii ni kubwa sana Kata zaidi ya 4,400 na Vijiji zaidi ya 10,000. Chombo cha pekee ambacho kinaweza kuwa karibu na wananchi kwa uhakika ni Serikali za Mitaa/Halmashauri za Wilaya. Chombo hiki lazima kipewe nguvu ya kifedha kimakusudi

Tunajua kuwa tayari Serikali Kuu imeshatumia sheria za kodi kupora kodi za ardhi, kodi ya majengo, kodi ya mabango, ushuru wa machinjio n.k. kutoka kwa Serikali za Mitaa. Kiinachotokea kwa sasa ni Serikali hizo/Halmashauri hazina OC, halmashauri zinakufa na hazina tena uwezo wa kuwahudumia wananchi.

6) Bajeti zote za Dk. Mpango na wenzake na serikali ya CCM kuanzia 2016/17, 2017/18 na sasa 2018/19 hazina mkakati na bajeti yoyote ya kuchangamsha PPP, achilia mbali sekta binafsi peke yake.

Inafahamika kuwa uchumi wan chi yoyote duniani haukuzwi na serikali, ni sekta binafsi ndiyo huhusika na ukuaji wa uchumi wa jumla, kazi ya serikali ni kujiunganisha na sekta binafsi na kuikabidhi sekta binafsi uendeshaji wa miradi mbalimbali – Utaratibu wa sasa wa serikali kuamini katika mitindo ya Uchumi wa Kijamaa na Utaifishaji wa Mali za Umma ni kaburi la uchumi wetu.

Tunaanza kurudia yale yale ambayo yaliangusha uchumi wa taifa hili – Sera za kijamaa hazitekelezeki katika dunia hii inayokimbizana na teknolojia za kisasa, lakini hata wakati taifa letu likiwa changa na lisilochangamka, sera za Ujamaa zilishindikana. Anayeendelea kumshauri Rais kuwa anaweza kurudisha kila njia ya uchumi au utekelezaji wa mioundombinu ya kiuchumi chini ya serikali, analiua taifa letu.

Bajeti ya sasa ya Dk. Mpango, na bajeti za miaka miwili iliyopita, hazina viashiria, mpango wala dalili ya mkakati wowote wa kiuchumi wa kukabiliana na ongezeko la watu. Mataifa mengi barani Afrika yameingia kwenye matatizo makubwa kwa sababu hayakuweka miundombinu ya kimazingira na kiuchumi ya kupokea ongezeko la watu.

Kwa mfano, kwa mujibu wa makisio ya Umoja wa Mataifa, ifikapo mwaka 2050 (miaka 32 tu kutoka sasa), idadi ya watanzania itakuwa mara mbili ya watanzania waliopo sasa – wakati huo taifa letu litakuwa na watu Milioni 100 na kabla ya mwaka 2100 taifa litakuwa na watu zaidi ya milioni 200.

Ili kuondoa athari za ongezeko la watu kwenye kizazi kianchokuja ni lazima taifa letu liwe na mkakati wa muda mrefu wa kusaidia kujenga mazingira rafiki kwa watu hao ikiwemo kuandaa miundombinu ya uhakika.

7) Wizara ya Fedha na Serikali viache kucheza na maisha ya wafanyakazi na wastaafu. Kama kuna makundi yameathiriwa sana na bajeti hii ya 2018/19 na bajeti mbili zilizopita ni wafanyakazi na wastaafu.

Makundi haya ni ya watu wanaojitolea au waliojitolea kulitumikia taifa letu kwa jasho kubwa lakini ni makundi ambayo yanaumizwa na kunyonywa kupita kiasi. The Civic United Front (CUF) kinaitaka serikali kulipa mara moja pesa za ongezeko la mishahara ya wafanyakazi ambalo lipo kisheria (Annual Statutory Income).

Ongezeko hili liliwekwa kimakusudi kisheria ili kuifanya serikali itimize wajibu wak, tangu serikali ya awamu ya tano ya JPM imeingia madarakani, utekelezwaji wa ongezeko hili la kisheria umepuuzwa na kudharauliwa bila kujali kuwa hili ni takwa la kisheria.

Tunajua kuwa serikali iko “bankruptcy” na inapumulia mashine (kwa mujibu wa takwimu tulizozionesha) na ndiyo maana imeshindwa kuwaongezea wafanyakazi mishahara kulingana na ukuaji wa uchumi, jambo ambalo ni aibu – sisi tunataka wafanyakazi walipwe fedha zao hizi za kisheria.

Na kwa uzito huo huo tunaisisitiza serikali kwamba mwaka huu wa fedha 2018/19 ihakikishe inalipa fedha za pensheni za kustaafu za wastaafu zaidi ya 7000 waliostaafu mwaka 2016 na 2017 ambao wamejazana mitaani bila kulipwa na ihakikishe kuwa wale wengine 3,000 wanaotarajiwa kustaafu mwezi Julai 2018, wanalipwa mafao na pensheni zao. Ni jambo la kusikitisha sana ikiwa serikali inakalia fedha za wazee hawa ambao hawana hata umri mrefu wa kuishi.

JULIUS MTATIRO,

MWENYEKITI WA KAMATI YA UONGOZI.

THE CIVIC UNITED FRONT (CUF),

Jumapili, 24 Juni 2018.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Chadema yamtaka Rais Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

KimataifaTangulizi

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the love  TUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

error: Content is protected !!