June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CRDB yaahidi neema

Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei

Spread the love

BENKI ya CRDB, imetangaza kuanza kuwahudumia watumishi walio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kuwalipa mishahara pindi serikali itakapochelewasha fedha zao kupitia benki hiyo. Anaandika Moses Mseti … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei, wakati wa semina ya kampeni ya ‘Ulipo Tupo’ kwa viongozi wa halmashauri zote za mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Semina hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo na viongozi wengine wa serikali.

Dk. Kemei amesema CRDB imekuwa ni miongoni mwa benki chache nchini zilizopewa jukumu la kuwahudhumia watumishi wa serikali kutokana na ufanisi walionao ikilinganishwa na benki nyingine.

“Kila mmoja anafahamu tulikuwa na benki moja ambayo ilipewa jukumu la kutunza fedha za serikali na kuwalipa watumishi wake,  sasa na CRDB nayo imeaminiwa na kupewa jukumu hilo, tunaahidi tutakuwa wabunifu na kulipa mishahara kwa wakati kulingana na tarehe tutakayokubaliana na halmashauri husika.

“Nataka kuweka wazi kwamba CRDB haitasubiri serikali iingize mishahara ya watumishi wake ndio tuwalipe, hapana. Tunazo fedha nyingi tutakuwa tunawalipa kwa fedha zetu na kisha serikali kutulipa,”amesema.

Amesema licha ya serikali kuwa na fedha pamoja na uwezo wa kulipa, lakini kuna changamoto nyingi na kuwahakikishia watumishi kulipwa mishahara na mikopo yenye masharti nafuu.

Naye waziri Ghasia, alipongeza kitendo cha CRDB kuamua kuwalipa mishaahara watumishi bila kujali kama serikali imeiingiza mishahara yao.

Amesema kutokana na kitendo hicho, tayari asilimia 80 ya halmashauri zimechagua na kukubali kupata huduma zao kutoka benki ya CRDB na kutoa wito kwa benki hiyo kutoziangusha  halmashauri zilizowamini na kuwapa dhamana ya kuwahudumia watumishi wake.

“Chombo chochote kinapopewa dhamana ya kuhudumia serikali kikiwa hakina mshindani kinafanya kazi kwa kubweteka ili kitoe huduma bora ni lazima kipate mshindani, sasa kimepata mpinzani.

“Nawashukuru kwa huduma mnazozitoa katika halmashauri, natamani siku moja nione benki ya CRDB inabeba dhamana ya kuihudumia serikali kwa asilimia 100, ”amesema Ghasia.

Amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote na zile ambazo hazijajiunga na huduma hiyo, kuwasaidia watumishi wao ili waweze kupata fursa za kupata mikopo binafsi ndani ya benki hiyo na kutatua matatizo yao.

Benki ya CRDB ina jumla ya matawi 35 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa sawa na asilimia 22 ya matawi yote ya benki hiyo hapa nchini.

error: Content is protected !!