SERIKALI ya Kenya, imepoteza jumla ya Ksh. 560 Bilioni (zaidi ya Tsh. 11 trilioni), tangu ilipokumbwa na mlipuko wa uonjwa wa corona (COVID-19) mwaka 2020. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa…(endelea).
Serikali ya nchi hiyo sasa imeongeza siku 60 kwa wananchi wake kukaa karantini, huku ikipiga marufuku mikutano ya kisiasa kwa siku 30 ili kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya corona.
Marufuku hiyo imetolewa na Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya leo Ijumaa tarehe 12 Machi 2021, wakati akitoa mwenendo wa maambukizi hayo na athari zake nchini humo.
Akitoa mwelekeo wa serikali hiyo kuhusu mapambano dhidi ya COVID-19, Rais Kenyatta ameagiza polisi kuhakikisha, marufuku hiyo inatekelezwa bila kujali vyeo vya watu.
Amesema, mtu yeyote akiwemo yeye, kama atakwenda kinyume na marufuku hiyo dhidi ya mikusanyiko ya kisiasa, atachukuliwa hatua za kisheria.
Na kwamba, serikali yake imeamua kuzuia mikutano ya siasa, kwa kuwa asilimia kubwa ya maambukizi yanatokea kwenye mikusanyiko ya kijamii na kisiasa ambapo watu wengi hawachukui tahadhari ya kuzuia maambukizi, ikiwemo kukaa mbali mbali.
“Kwa kutambua kuwa ueneaji wa ugonjwa wa COVID-19 ndani ya mipaka yetu umechangiwa na mikusanyiko mikubwa ya kijamii na mikutano ya kisiasa, Ninaelekeza kwamba, mikusnayiko ya kisiasa ni marufuku kwa kipindi cha siku 30 kuanzia usiku wa leo.”
“Yeyote atakayevunja maagizo ya kutofanya mikutano, ikiwa pamoja na mimi, atachukuliwa hatua za kisheria,” ameonya Rais Kenyatta.
Amesema, shughuli za mazishi nchini humo, zinatakiwa kufanyika ndani ya saa 72 baada ya mtu kufariki, huku watakaoruhusiwa kushiriki wasizidi 100.
Pia, Rais Kenyatta ameagiza migahawa na baa zifungwe saa 9 alasiri.
Aidha, amesema serikali imepoteza mapato kiasi cha KSh. 560 bilioni tangu ilipokumbwa na janga hilo mwaka 2020.
Amesema, ukuaji uchumi wa Kenya unatarajiwa kushuka hadi kufikia asilimia 7 kwa mwaka, kama hatua madhubuti za kuimarisha uchumi hazitachukuliwa.
Kenya ilianza kujiweka karantini tangu Machi 2020, baada ya kuripoti kisa chake cha tatu cha ugonjwa wa COVID-19.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mamlaka za Kenya, tangu Taifa hilo likumbane na mlipuko huo, watu 110,356 wamethibitika kuambukizwa COVID-19, ambapo 87,903 walipona huku 1,898 wakipoteza maisha.
Leave a comment