WAKATI dunia ikiendeleza mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19), Taasisi ya My Legacy nchini Tanzania, imetoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanachukua tahadhari ya ugonjwa huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taasisi hiyo imesema, kila mmoja anapaswa kunawa mikono na maji tiririka na sabani ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo ambao bado haujapata tiba.
My Legancy imetoa kauli hiyo leo Jumatano, tarehe 14 Julai 2021, siku ambayo pia, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo.
Rais Samia amekuwa akisisitiza, kila mmoja kuvaa barakoa na kunawa mikoni na maji tiririka ili kujikinga na ugonjwa huo ambao upo nchini.
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Fortunata Temu, akizungumza Dar es Salaam amesema, wameandaa matenki ya maji na sabuni kwa ajili ya shule zilizo katika kata tatu za wilaya ya Kinondoni, jijini humo.
Amesema, kata hizo ni Kawe, Kunduchi na Wazo ambazo zipatewa matenki na sabuni ili kuhakikisha wanafunzi wananawa mikono kwa maji tiririka.

“COVID-19 ni janga kubwa ambalo halina dawa mpaka sasa na zaidi tunahitaji kuchukua hatua. Kunawa si kunawa tu, lazima unawe kwa njia sahihi,” amesema Fortunata.
Akizungumzia ugawaji wa manteki hayo amesema, “tumeona tuanzie na shuleni kwani shule wanatumia muda mwingi sana na idadi ya wanafunzi ni wengi. Tukiwajengea wanafunzi mazoea ya kunawa, hata wakirudi nyumbani, wanakuwa mabalozi wazuri.”
Amesema, vigezo vilivyotumika kupata shule zitakazonufaika na mpango huo ni shule kuwa na zaidi ya wanafunzi 500.
“Katika kutembelea kwetu, tumeona shule ina zaidi ya wanafunzi 2000, sasa tutaanza na Wilaya ya Kinondoni na ujumbe wa kunawa mikono wa ‘nawa mikono kwa afya, boresha makazi’ ukiwaingia vizuri wanafunzi, tutafanikiwa,” amesema.
Leave a comment