May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

COVID-19: CUF, ACT-Wazalendo ‘waifuata’ serikali

Ado Shaibu, Katibu Mkuu ACT-Wazalendo

Spread the love

 

SIKU chache kupita baada ya viongozi wa Kanisa Katoliki Tanzania kutoa mwongozo kuhusu kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya corona, Chama cha Wananchi (CUF) na ACT-Wazalendo vimeitaka serikali kuongeza umakini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

CUF na ACT-Wazalendo wameitaka Serikali kuongeza jitihada katika kukabiliana na athari corona kwa maslahi ya Watanzania. Wito wa vyama hivyo umetolewa leo Ijumaa tarehe 29 Januari 2021.

Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo ameiomba serikali iwajibike katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo, ili kuokoa maisha ya Watanzania.

“Chama kitachukua hatua za kuitaka serikali kuwajibika inavyostahiki katika mapambano dhidi ya virusi hivi, ili kuokoa maisha ya Watanzania yasizidi kupotea,” amesema Ado.

“Hatua ambazo serikali imezichukua tangu mlipuko wa kwanza mwaka jana na hata sasa tunavyokabiliana na mlipuko wa pili, haziridhishi,” amesema Ado
“Tuzingatie na kufuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na kupambana na janga la virusi hivi. Janga la virusi vya corona haliwezi kuisha nchini kwa kujidanganya kuwa halipo. Tuchukue tahadhari,” amesema Ado.

Mhandisi Mohamed Ngulangwa, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma CUF (kulia)

Mohamed Ngulangwa, Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mahusiano na Umma CUF amesema, chama hicho kinaunga mkono msimamo wa Rais John Magufuli wa kutowaweka karantini wananchi.

Pamoja na msimamo wa chama hicho, amesema serikali ya Rais Magufuli inapaswa kufuata njia za kisayansi katika kukabiliana na janga hilo.

“Pamoja na kuunga mkono matumizi ya njia sahihi za asili za kupambana na corona, CUF tunatoa wito kwa serikali kufuata njia za kisayansi katika masuala ya corona ikiwa ni pamoja na kutafakari upya juu ya msimamo uliotolewa kuhusu chanjo,” amesema Ngulangwa.

Ngulangwa amewashauri wataalamu wa afya, kufanya tathimini ya ubora wa chanjo zitakazosaidia Watanzania kukabiliana na ugonjwa huo.

“Tunashauri wataalam wetu wajipange kutathmini ubora wa chanjo tunazoweza kutumia Tanzania dhidi ya corona, badala ya kuzikataa kienyeji. Aidha serikali iweke utaratibu mwepesi na usio ghali wa kupima corona,” amesema.

Hivi karibuni, Askofu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alituma waraka kwa maaskofu akiwataka kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya corona.

Askofu Nyaisonga aliwashauri maaskofu wa kanisa hilo kupaza sauti zao katika kuwaongoza waumini juu ya mapambano dhidi ya Covid-19.

error: Content is protected !!