May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

COVID-19: Baada ya miezi 9, Kenya yafungua shule

Msemaji wa Ikulu ya Kenya, Kanze Dena

Spread the love

BAADA ya miezi tisa ya kufungwa kwa shule nchini Kenya, leo Jumatatu tarehe 4 Januari 2021, shule hizo zimefunguliwa na kuanza masomo. Inaripoti mitandao ya kimataifa…(endelea).

Shule hizo zilifungwa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona (COVID-19), ambapo sasa changamoto inayowakabili ni msongamano wa wanafunzi kwenye darasa moja.

George Magoha, Waziri wa Elimu nchini humo, amepita katika shule mbalimbali kuangalia mapokezo mapya ya wanafunzi kulingana na mwongozo wa wizara yake katika kukabiliana na maambukizi mapya.

Taarifa zaidi zinaeleza, miongoni mwa sababu za msongamano wa wanafunzi kwenye darasa moja ni kutokana na baadhi ya shule binafsi kufungwa, kutokana na kushindwa kuziendesha ikiwa ni matokeo hasi ya COVID-19.

Hivyo, wazazi wa watoto hao, wamelazimika kusaka shule zingine awali ili watoto wao wasiache nyuma pale masomo yatakapoanza na kujikuta darasa moja lina watoto wengi.

Kenya kama baadhi ya nchi nyingine Afrika, zimeshambuliwa na virusi vya corona na kusababisha madhara makubwa ikiwemo ya uchumi.

Mpaka kufikia leo, katika nchi za Afrika Mashariki, Kenya inaongoza kwa kuwa na maambukizo 96,802 ambapo waliopona wamefika 79,073 na waliofariki ni 1685.

Kwa Afrika, Afrika Kusini inaongoza kwa kuwa na maambukizo milioni 1.1, waliopona 903,679 na waliofariki wakiwa 29,577.

Morocco inashika nafasi ya pili Afrika ikiwa na maambukizo 443,146, waliopona 413,393 na vifo vikiwa 7,485.

Maambukizo ya corona sasa yamefikia milioni 85.5 ambapo waliopona ni milioni 60.4 na waliopoteza maisha wamefika milioni 1.8.

Hadi leo hii, Marekani inaongoza kwa maambukizo mengi duniani yaliyofikia milioni 21.1, waliofariki 360,078 na waliopona milioni 12.4. India inashika nafasi ya pili ikiwa na maambukizo milioni 10.3, waliopona milioni 9.9 na waliofariki wakiwa 149,686.

Brazil ina maambukizo milioni 7.7 ikiwa nafasi ya tatu, waliofariki kutokana na ugonjwa huo wakiwa 196,018 na waliopona milioni 6.8.

error: Content is protected !!