May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la COVID-19: Askofu Niwemugizi ataka ukweli uanikwe

SEVERINE Niwemugizi, Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara

Spread the love

 

SEVERINE Niwemugizi, Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara amehoji, “changamoto ya upumuaji ni kitu gani?” Anaripoti Mwandishi Wetu, Ngara…(endelea).

Askofu Niwemugizi amehoji leo Jumanne tarehe 16 Februari 2021, katika adhimisho la miaka 24 ya Uaskofu, yaliyofanyika katika Parokia ya Mt. Fransisco wa Assizi, Kanisa Kuu la Ngara Mjini, jimboni humo.

Kiongozi huyo wa kidini, alikuwa akizungumzia mazingira ya sasa ya dunia kutokana na janga la virusi vya corona (COVID-19).

Askofu Niwemugizi ameeleza kuwa, watu wanakufa lakini kinachoelezwa sababu za vifo hivyo ni changamoto ya upumuaji.

Amesema, kwa sasa taarifa za janga la dunia ndani ya mipaka ya Tanzania zina utata, amewataka viongozi kuwa wakweli.

“Sasa hivi katika nchi yetu iko hali ya utata, watu wanakufa kufa tu. Huko duniani kule wanasema kuna corona jamani, hapa wanasema ahaha, hapa kuna shida ya kupumua sio corona. Shida ya kupumua ni nini?

“Vitu vya aina hiyo tunajua ukweli ni huu sisi tunasema, bwana anakukemea tujiepushe na tabia ya mafarisayo ambayo ni unafiki,” amesema Askofu Niwemugizi.

Kiongozi huyo wa kiroho, amewaomba viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla kusema ukweli bila kuupindisha.

“…na kama unahubiri Injili, Bwana kakutuma kusema ukweli halafu unasema uongo, adhabu utakayopewa ni kubwa,” amesema Askofu Niwemugizi.

Dk. Hassan Abbas, Msemaji wa Serikali

Dk. Hassan Abbasi, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania hivi karibuni akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), alisema serikali imefanikiwa kudhibiti Covid-19.

Wakati Dk. Abbasi akitoa taarifa hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) hivi karibuni, alisema changamoto ya upumuaji ni ya kawaida na ilikuwepo kabla ya mlipuko wa Covid-19.

Dk. Mollel alisema, watu wanakuza tatizo hilo, kwa kuwa lilikuwepo miaka mingi ambapo kwa asilimia kubwa lilikuwa linasabishwa na ugonjwa wa Nimonia.

error: Content is protected !!