Friday , 24 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Corona: Zitto aainisha mambo 7 kwa JPM
Habari za Siasa

Corona: Zitto aainisha mambo 7 kwa JPM

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo
Spread the love

ZITTO Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, amemwandikia barua ya ushauri Rais John Magufuli iliyohusu namna ya kuukabili ugonjwa unaotokana na virusi vya corona (COVID-19). Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam…(endelea).

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 29 Machi 2020, Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini amesema, amechukua hatua hiyo kama wajibu katika kumshauri Rais Magufuli kuliweka taifa katika hali salama.

“Juzi tarehe 27 Machi 2020, nimemuandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli…., kuhusiana na namna bora ya kudhibiti na kukabiliana na virusi vya KORONA hapa nchini. Barua hiyo ilifikishwa jana,” amesema.

Kwenye barua hiyo, Zitto amewataka wananchi kuhakikisha wanatii maelezo ya wataalamu na si ya kisiasa kwa mastahi na usalama wa Taifa na kwamba, ugonjwa hu ni mpya, hiyo taarifa nyingi haizijulikani.

“Wanasayansi wanasema, kinachojulikana mpaka sasa kuhusu ugonjwa wa corona ni asilimu 15 mpaka 20 tu. Kila wakati tunapata taarifa mpya, mfano; muda mgonjwa anapoanza kuugua ili kuwa siku 1-14 lakini sasa sasa inaweza kuwa siku 24.

“Pili: njia kuu iliyothibitishwa ni majimaji njia ya hewa, hata hivyo tafiti zinazoendelea zinaeleza, ugonjwa huu unaweza kuambukizwa kwa njia zingine, kama njia ya kuvuta hewa ama kinyesi. Hatupaswi kupuuza kabisa njia mbalimbali za maambukizi.”

Katika barua hiyo aliyomwandikia Rais Magufuli, ameainisha maeneo saba ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kwa karibu zaidi ili kunusuru hali mbaya inayoweza kutokana na virusi vya corona. Maeneo hayo ni:-

Kwanza: Umoja wa kimataifa. Amesema, hakuna wakati nchi yetu inahitaji umoja kama wakati huu, “Mheshimiwa Rais akiwa ndiye mkuu wa nchi ana wajibu mkubwa wa kutuweka Watanzania pamoja kwa vitendo.”

amesema, Watanzania tukiwa wamoja, tutaweza kupambana na virusi vya corona na kushinda pamoja na ikibidi kushindwa tushindwe pamoja.

Pili: Wataalamu. Kiongozi huyo ameshauri, damu ya kila mwanadamu inaweza kupata maambukizi ya virusi hivyo, “ni muhimu sana sisi viongozi kuepuka kutoa maneno ya jumla jumla ambayo yanawapa wananchi wetu matumaini hewa, na hivyo kusababisha hatari zaidi.

“Tutoe nafasi kwa wataalamu wa afya kutuongoza katika mapambano haya ya kudhibiti ugonjwa wa corona. Ni lazima sasa, maneno tunayoyasema kwa umma na maamuzi tunayoyachukua katika kudhibiti mlipuko huu yazingatie ushauri wa wataalamu badala ya imani zetu au fikra zetu.”

Tatu: Kupima. Ameshauri nchi kuweka mazingira mazuri ya kupima ili kujua kiwango cha athari na namna ya kukabili ugonjwa huo.

“Uzoefu wa Nchi kama Ujerumani umeonesha, kuwa licha ya maambukizi kuwa makubwa, wamefanikiwa kuzuia vifo kwa sababu ya kampeni kubwa ya kupima watu.”

Amesema, kasi ya nchi kupima ni ndogo mno na inategemea msaada wa Mashirika ya Kimataifa kama Center for Disease Control and Prevention (CDC) na tajiri wa China Jack Ma ambaye ni mmiliki wa Alibaba.

Nne: Uwazi. Amesema, uwazi wa takwimu za maambukizi, maambukizi mapya, wagonjwa mahututi na vifo ni muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huu.

“Uwazi umesaidia sana nchi kama Korea ya Kusini, na usiri umeathiri kwa kiwango chake nchi kama China. Nimemnasihi Mheshimiwa Rais kwamba, tusione aibu hata kidogo kuweka wazi idadi ya wagonjwa wa corona kwani kuna faida zaidi kuliko kuficha.”

Tano: Kuepuka maelezo yanayopingana. Ameishauri serikali kuchukua hatua muafaka kufunga shule na vyuo kote nchini ili kuzuia maambukizi.

Amehoji, serikali inatuma ujumbe gani kwa wananchi? “hasa watoto wetu wanapoona wao wamefunga shule lakini viongozi wanahutubia makumi ya watu hadharani? Wanapata ujumbe gani wanapoona Bunge linaendelea na vikao?

“Wanapata picha gani wanapomuona Rais wao anaendelea na mikutano yenye mikusanyiko? Nimemuomba kwa heshima zote Mheshimiwa Rais, hatua zichukuliwe kusimamisha vikao vyote vya Kiserikali ikiwemo Bunge, Mahakama.”

Sita: Mahabusu na wafungwa. Zito amemshauri Rais Magufuli kwamba, Mwendesha Mashtaka wa Serikali aondoe zuio la dhamana kwa kesi zote ambazo kazuia dhamana na zile ambazo hazina dhamana kisheria lakini upelelezi bado unaendelea.

Ameshauri, watuhumiwa wasubiri upepelezi wakiwa majumbani mwao ili kupunguza msongamano magerezani.

Saba: Shughuli za kila siku. Amesema, kwa vyovyote vile Tanzania haiwezi kuendelea na uendeshaji wa mambo kama yalivyozoeleka wakati huu.

“Ninafahamu madhara makubwa ya kiuchumi na kwa maisha binafsi ya watu wetu, iwapo tukizuia shughuli za kila siku kama ilivyofanyika nchi nyengine kama vile Afrika ya Kusini na India.

“Hata hivyo, tunaweza kuwa na njia mbadala ya kuzuia maambukizi bila kuathiri sana shughuli za kila siku za watu wetu,” amesema Zitto.

Nane: Kuhami uchumi: amesema, hatua zinazochukuliwa kuzuia mashambulizi ya corona lazima zitaathiri uchumi wa nchi.

“Baadhi ya watendaji walioko serikalini ni wataalamu wa hesabu za uchumi haswa Modeli za mahusiano ya sekta za uchumi. Nimemsihi sana Rais kuwa timu ya wataalamu wa uchumi nchini iundwe na kuanza kazi mara moja,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Biteko awataka makatibu mahsusi kujiendeleza, kuwa kielelezi cha huduma bora

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia muonee huruma Dk. Phissoo

Spread the loveRAIS wangu mama Samia, wiki iliyopita baada ya kuwa nimekuandikia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 63 ya Uhuru bila katiba ya wananchi

Spread the loveWAFUASI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanaharakati...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Serikali mbili ni sera ya CCM, si mkataba wa Muungano

Spread the loveMUUNGANO kati ya Tanganyika na Zanzibar uliotimiza miaka 60 tangu...

error: Content is protected !!