UGONJWA unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) umeendelea kutikisa nchini Kenya, baada ya watumishi wanne wa Ikulu kubainika kuwa na ugonjwa huo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea)
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu tarehe 15 Juni 2020 na Msemaji wa Ikulu ya Kenya, Kanze Dena imesema, watumishi hao wamebainika kuwa na corona baada ya watumishi wote wa Ikulu kupimwa.
Dena amesema, watumishi hao wamepelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi na uangalizi.
“Uchunguzi ulifanyika kwa watumishi wote akiwemo Rais (Uhuru Kenyatta) na familia yake,” amesema Dena.
Katika taarifa yake, Dena amesema, Rais Kenyatta na familia yake wako salama, hawana maambukizo ya COVID-19.
Taarifa hiyo ya Dena imetolewa muda mfupi baada ya ile ya Katibu wa Baraza la Mawaziri la Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe inayoonyesha wagonjwa wapua 133 wamebainika ndani ya saa 24 zilizopita.
Kenya imekuwa na utaratibu wa kutoa taarifa za maambukizo ya COVID-19 kila siku.
Amesema, wagonjwa wa corona wamefikia 3,727.
Kangwe amesema, wagonjwa waliopona wamefikia 1,286 baada ya wagonjwa 33 kuruhusiwa kutoka hospitalini ndani ya saa 24 zilizopita huku mgonjwa mmoja akipoteza maisha hivyo kufikisha idadi ya waliofariki kwa ugonjwa huo wakiwa 104.
Hali ya maambukizo duniani ya COVID-19 kwa mujibu wa mtandao wa worldometer yanaonyesha yamefikia milioni 8.02, waliopona ugonjwa huo wakiwa milioni 4.04 na waliopoteza maisha wakiwa 436,218.
Taifa la Marekani limeendelea kuongoza duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi, milioni 2.16, waliopoteza maisha 117,859 huku waliopona wakiwa 870,077.
Leave a comment