December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Corona yaisukuma mahakama kubadili mfumo

Spread the love

PROFESA Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania, amesema mhimili wa mahakama umeanza kutumia mfumo wa Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika uendeshaji wa shughuli zake, ikiwa sehemu ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona (COVID-19). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 24 Machi 2020, Prof. Juma amesema mfumo huo utasaidia kupunguza mikusanyiko katika mahakama, jambo litakalosaidia kudhibiti ueneaji wa ugonjwa huo.

“Katika uendeshaji wa shughuli za kimahakama wakati huu dunia inapambana  na tahadhari ya janga la Corona, mahakama ya Tanzania ni taasisi ya umma ambayo inatakiwa kutekeleza tahadhari inayotolewa na serikali.

Tunaanza kutumia Tehama zaidi na kuongeza maeneo ya matumizi ya Tehama, tunadhani matumizi ya Tehama ni zaidi hasa katika kuondoa misongamano,” amesema Prof. Juma.

Prof. Juma amesema kuanzia sasa usajili na uendeshaji wa kesi utafanywa kwa njia ya kielektroniki, pia, taarifa za kimahakama zitatolewa kupitia njia ya mtandaoni ikiwemo simu na barua pepe.

“Pamoja na matumizi ya TEHAMA katika usajili wa mashauri kwa njia ya elektroniki, mfumo wa kufungua na  kuendesha kesi kwa njia ya elektroni ni wakati muhimu wa kutumia sana. Upatikanaji wa taarifa za kimahakama kupitia njia ya simu, tutapitia hivyo kuliko wadawa kuja mahakamani kufuata taarifa, “ amesema Prof. Juma na kuongeza:

“Tutatumia barua pepe na tovuti yetu kutoa taarifa mbalimbali, wananchi wajaribu kubadilisha maisha watumie hizi nyenzo ambazo zipo , hii mifumo inaruhusu mwananchi kupata huuma hizi bila kufika katika mahakama zetu .”

Prof. Juma amewataka wananchi wanaotaka kufungua mashauri, kutumia kanuni za kufungua mashauri kwa njia ya mtandao.

“ Tunaomba wadau wote kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Tanzania ili kuendeleza mapambano na kujikinga na ugonjwa wa Corona.Kwa sasa kuna mfumo wa kusajili na kuratibu, mfumo huu umeunganishwa na mfumo wa malipo serikalini, kwa hiyo malipo ya kufungua mashauri yatafanyika bila kuja mahakamani, kuna mfumo wa kusimamia na kutambua mawakili halali,” amesema Prof. Juma.

error: Content is protected !!