Thursday , 25 April 2024
Home Habari Mchanganyiko CMA yaamuru Manji kulipa mamilioni waandishi wa habari
Habari Mchanganyiko

CMA yaamuru Manji kulipa mamilioni waandishi wa habari

Yusuf Manji
Spread the love

TUME ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Kanda ya Dar es Salaam- Temeke imeiamuru kampuni ya Quality Group Limited kuwalipa waandishi wake wa habari wa zamani 23 iliowaachisha kazi mwaka 2017, jumla ya Sh.232.32 milioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tume hiyo inayofanya kazi kama Mahakama ya Mwanzo ya Migogoro ya Kazi, iliiamuru kampuni hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu, Yusufu Manji, kuwalipa waandishi hao kiasi hicho cha fedha, baada ya kuridhika ilivunja mikataba baina yao kwa kuwaachisha kazi bila sababu maalumu.

Ilifikia uamuzi huo baada ya wanahabari hao kufungua shauri la mgogoro wa kikazi, wakipinga uamuzi wa kampuni hiyo kuwaachisha kazi kabla ya muda wa mikataba yao wa miaka miwili waliyosainiana kuisha.

Wanahabari hao walikuwa wakifanya kazi katika gazeti la JamboLeo, lililokuwa likimilikiwa na kampuni ya Manji ya Quality Media Ltd, ambapo waliachishwa  huku mlalamikiwa akitoa sababu alikuwa amesikia mambo mazuri kuwahusu wao.

Katika shauri hilo, wanahabari hao, Joseph Lugendo na wenzake 22 walidai waliajiriwa na mdaiwa huyo kwa nyakati tofauti kwa mikataba ya miaka miwili, lakini tarehe 19 Septemba  2017 hata kabla muda wa mikataba yao haujaisha, mdaiwa aliwaachisha kazi.

Hivyo, pamoja na mambo mengine, walikuwa wakiiomba tume hiyo iiamuru kampuni hiyo iwalipe fidia kwa uvunjai wa mkataba kabla ya muda na malipo ya mishahara ya miezi iliyokuwa imesalia kabla ya mikataba yao kufikia mwisho.

Pia, walikuwa wakidai nyongeza ya mishahara kulingana na makubaliano ya kimkataba,  cheti cha huduma, fidia ya madhara ya jumla, malipo ya mishahara hadi tarehe ya uamuzi wa shauri hilo na  ujira maalumu (kamisheni).

CMA katika tuzo (uamuzi) alioutoa tarehe 24 Juni 2019, Msuluhishi aliyefahamika kwa jina la Kokusiima L, amekubalina na madai na maelezo ya ushahidi wa walalamikaji hao kuwa kilichofanywa na mlalamikiwa ni uvunjaji mkataba kwani hakuzingatia sheria.

Alisema hapakuwa na sababu halali ya usitishaji wa mikataba ya walalamikaji kabla ya muda kuisha. Aliongeza kuwa sababu aliyoitoa mlalamikiwa ni kinyume cha kifungu cha 8(1) (d) cha Kanuni za Ajira na Mahusiano Kazini (Kanuni za Utendaji Bora) za mwaka 2007.

Msuluhishi alifafanua kuwa sababu aliyoitoa kwamba amesikia kitu kizuri kutoka kwa wafanyakazi wenzao ni tata, kwani hakuna namna ambavyo mtu anaweza akaachishwa kazi kwa kusikia habari nzuri kuhusu yeye. Kwa mujibu wa  CMA, mlalamikiwa hakuzingatia sheria ambayo inataka kutoa taarifa ya siku zisizopungua 28.

Hata hivyo, Msuluhishi Kokusiima alisema kwa kuwa mikataba ya walalamikaji ilikuwa ni ya muda maalumu, basi kanuni ya kuachishwa kazi kusiko kwa haki haiwezi kutumika na kwamba walalamikaji wana haki ya kulipwa mishahara ya miezi ilioyokuwa imebakia tu.

“Kwa hiyo katika kesi hii,  kushindwa kwa mlalamikiwa kuzingatia masharti ya mkataba hususan kifungu cha muda wa usitishaji mkataba, anawajibika kumlipa kila mlalamikaji mishahara kwa miezi iliyokuwa imebakia ya mkataba wa ajira,” alisema Msuluhishi

“Mdaiwa anawajibika kuwalipa walalamikaji (wote kwa ujumla) jumla ya Sh232,324,172.96. Pia kila mlalamikaji sharti apewe hati cheti safi cha huduma. Walalamikaji walishindwa kuthibitisha madai mengine hivyo yanatupiliwa mbali.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!