January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CM-TANZANIA yapatiwa usajili wa muda

Spread the love
MSAJILI wa Vyama Vya Siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi leo amekipa usajili wa muda mfupi chama kipya kinachoitwa Chama cha Maadili na Uwajibikaji  (CM-TANZANIA). Anaandika Sarafina Lidwino.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake  kabla ya kukabidhi hati ya usajili, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza amesema, chama hicho kipya kilianza kuomba usajili tangu mwaka 2014.
Amesema, na sasa anakipa usajili wa muda mfupi wa miezi mitatu na kisha kitapatiwa usajili wa kudumu baada ya kutimiza matakwa ya usajili wa kudumu.
Nyahoza pia amekitaka chama hicho kutambua wajibu wake ndani ya miezi hiyo mitatu ikiwa ni pamoja na kuitisha mikutano ya kukitambulisha chama chao, watafute wanachama 2000 kwa kila mkoa ikiwemo na Zanzibar, chama kiwe na ofisi nzuri pamoja viongozi wa chama watakaoridhiwa na wananchama.
Pia amekitaka chama kiwe na bendera, viongozi wa chama waisome sheria ya vyama vya siasa pia wawe na ushawishi kwa wananchi ndipo warudi tena kwa ajili ya usajili wa kudumu.
Jaji Mutungi baada ya kukabidhi hati ya usajili wa chama hicho, amewasisitiza viongozi wa chama kuzingatia na kuheshimu makubaliano ya vikao ili kuepusha mtafaruku kama vyama vingine vya siasa.
Pia ametoa ushauri kwa vyama vya siasa kufanya siasa  na sio kufanya harakati katika vyama vyao.
“Kuna vyama vingine hapa nchini vinatofautiana kofia tu lakini vinafanana kila kitu na mambo yao ni yale yale. Naomba nyinyi mkawe tofauti na vyama vingine,” amesema Mutungi.
Laban Nkembo, Mwenyekiti wa CM- Tanzania wakati wa kukabidhiwa hati ya usajili wa muda amesema, “hiki si chama cha upinzani, hiki kinaunga mkono Chama cha Mapinduzi.” Hata hivyo hakuwa tayari kujibu maswali mengine zaidi.
error: Content is protected !!