August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Clinton, tumaini jipya la wanawake

Spread the love

HILLARY Clinton, mke wa rais wa 42 wa taifa la Marekani Bill Clinton ameidhinishwa kuwa mgombea urais wa chama cha Democrat cha nchini humo huku akiweka rekodi ya kipekee, anaandika Pendo Omary.

Bi. Clinton mwenye umri wa miaka 68, anakuwa mwanamke wa kwanza nchini Marekani kupitishwa kuwania Urais tangu kuanza kwa mfumo wa demokrasia nchini humo yapata karne mbili zilizopita.

Hatua hiyo inafungua ukurasa wa matumaini kwa mamilioni ya wasichana na wanawake katika uongozi wa ngazi ya juu katika siasa nchini Marekani na duniani kote.

“Siamini kama tumefanikiwa kuweka ufa mkubwa zaidi katika dari hili la kioo.” Amesema Bi. Clinton katika ujumbe wa video uliorekodiwa Jumanne wiki hii huku akiongeza;

“Iwapo kuna wasichana wadogo huko ambao hawajalala na wananitazama, ningependa kuwaambia, huenda nikawa rais wa kwanza mwanamke Marekani na mmoja wenu anaweza kunifuatia.”

Kauli hiyo inatajwa kuwa ni ya kutia moyo na kuhamasisha harakati za kuwawezesha wasichana na wanawake kuwania nafasi kubwa za uongozi hasa katika mataifa makubwa ikiwemo Marekani.

Hillary Clinton amepitishwa kuwania urais nchini Marekani ikiwa ni miaka takribani 16 tangu mume wake Bill Clinton amalize muhula wake wa pili katika nafasi ya urais wa taifa hilo mnamo mwaka 2000.

Bi. Clinton atakabiliana na Donald Trump mgombea urais kutoka chama cha Republican katika uchaguzi utakaofanyika Novemba mwaka huu. Iwapo atashinda uchaguzi huo, atakuwa rais wa 45 wa Marekani lakini pia mwanamke wa kwanza kuongoza taifa hilo.

error: Content is protected !!