August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Chozi’ la Meya Jacob kwa Rais Magufuli

Spread the love

“KOSA letu ni lipi kwenye nchi hii? Ni kuwa wapinzani?” Ni sauti ya Boniface Jacob, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni akilalama. Anahoji na kulalamikia hatua ya Rais John Magufuli kuipora manispaa hiyo umiliki wa eneo la Magomeni Kota na kulirejesha serikali kuu, anaandika Charles William.

Meya huyo amezungumza na wanahabari baada ya kunyimwa nafasi ya kuzungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika eneo la Magomeni Kota, ambapo Rais Magufuli aliwahutubia waliokuwa wakazi wa eneo hilo, akitangaza kuifutia hati ya umiliki wa eneo hilo manispaa ya Kinondoni.

Kabla ya Meya Jacob kuzungumza na wanahabari, maofisa usalama walifika na kumuhoji, walihofia kuwa angetoa maneno ya kumkashifu rais, kufautia uamuzi wake wa kulichukua eneo hilo kutoka manispaa hiyo.

“Hati imefutwa bila sisi kusikilizwa, Rais alipomtuma Waziri Lukuvi aje kuongea na sisi hakuja, badala yake vikao vya kushughulikia jambo hilo vikafanyika wizarani na katika ofisi ya Makonda. Wangeniita hata mimi, wangemwita hata mwenyekiti wa Mipango miji lakini hawakufanya hivyo.

Ningepata nafasi ningemwambia rais kuwa wanaokuzunguka kuna ukweli wanauficha na hao ndiyo wametuma vyombo vya ulinzi vije kunizuia nisiongee na vyombo vya habari.” Ameeleza Jacob kwa uchungu.

Akieleza hasara ambayo manispaa hiyo imepata baada ya Rais Magufuli kuamua kuinyang’anya manispaa hiyo eneo hilo, amesema manispaa imepoteza jumla Sh. 12 bilioni, huku akifafanua kuwa;

“Manispaa ilishaingia mkataba na mwekezaji wa Blue Marine na kampuni ya ujenzi ya Gulf GM, aidha Sh. 2 bilioni zilishatumika kuchora ramani na Sh. 700 milioni zilitumika kila mwaka kuwalipa fidia ya  pango waliokuwa wakazi wa eneo hilo kwa miaka mitano sasa.”

Meya Jacob ameeleza ‘dhoruba’ wanayokumbana nayo mameya wanaoongoza maeneo ya miji kwa tiketi ya vyama vya upinzani, na kusema ipo hatari ya kuporwa maeneo yote nyenye miradi mikubwa ya maendeleo kwasababu za kisiasa zaidi.

“Wiki tatu zilizopita, Meya wa Moshi alikuwa hapa kufuatilia saini ya waziri WA TAMISEMI ya mradi kama huu, na kwa miaka sita sasa wanafuatilia hiyo saini nikawambia ndugu zangu kuipata hiyo saini sahauni. Hapa ni siasa kwanza.

Wataporwa Arusha, Mbeya, Moshi na Dar miji mikuu yote ambayo mameya wa Ukawa wanaongoza.” Amesema.

 

error: Content is protected !!