June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chiza: Kigoma imepata milioni 946/-

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji na Uwezeshaji), Mhandisi Christopher Chiza

Spread the love

SERIKALI imesema kuwa, kupitia mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, Mkoa wa Kigoma umepata mikopo yenye thamani ya Sh. 946.49 milioni, ambazo zimewanufaisha wajasiriamali 1,407.

Kwamba, kati ya wajasiriamali hao, 353 wanatoka Kigoma Mjini, 827 wanatoka Kasulu, 207 wanatoka Kigoma Vijijini na 20 wanatoka Kibondo.

Takwimu hizo, zimetolewa leo bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji na Uwezeshaji), Mhandisi Christopher Chiza, wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Josephine Genzabuke (CCM), aliyetaka ufafanuzi wa idadi ya wananchi walionufaika.

Chiza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (Tamisemi), amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2006/2007, serikali ilianzisha mpango wa uwezeshaji.

Amesema mpango huo, uliwalenga wananchi walalahoi kwa kuinua uchumi wao pamoja na kuongeza ajira kwa kutoa mikopo kwa masharti nafuu.

“Masharti ya kupata mikopo hii si magumu ikilinganishwa na ile inayotolewa na mabenki kwa sababu riba inayotozwa kwa mikopo hii ni asilimia 10 ikilinganishwa na riba inayotozwa na mabenki ambayo ni zaidi ya asilimia 20.

“Aidha, wananchi wanaopewa mikopo kutokana na mfuko huu hawahitajiki kuwa na dhamana kama zile zinazotakiwa na benki,” amesema Chiza.

Ili kufanya mpango huo uwe endelevu, serikali imepanga kufanya tathmini ya kina katika mwaka wa fedha ujao ili kubaini vikundi na changamoto zilizojitokeza.

error: Content is protected !!