January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Cheyo awachafua UKAWA

Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo

Spread the love

JOHN Momose Cheyo, mbunge wa muda mrefu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, amepiga kampeni chafu dhidi ya wabunge wanaotokana na vyama vilivyounda UKAWA akitaka wasirudi bungeni. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Akijijengea uhalali wa kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa Oktoba 25, kwa kujiita ni muadilifu na mzalendo, Cheyo ambaye ni mbunge wa Bariadi Mashariki, alisema yeye amebaki bungeni kwa sababu anaamini mbunge hawezi kuzuia majukumu ya serikali.

Mbunge huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa chama alichoasisi tangu 1992 cha United Democratic Party (UDP), alieleza hayo leo alipokuwa akichangia muswada wa sheria ya kuunda Tume ya Utumishi ya Walimu, uliowasilishwa bungeni na Waziri wa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kwa niaba ya Waziri Mkuu.

Cheyo alisema wakati akiamini kuna shauku ya watu kujua ni kwanini yeye hakutoka bungeni kama walivyofanya wabunge wengine wa kambi rasmi ya upinzani, anachoamini ni kwamba huwezi mtu kwenda Ikulu ukamzuia Rais kufanya kazi ya kuongoza serikali.

Alisema haiwezekani bunge likaizuia serikali kutimiza majukumu yake. Badala yake, akasema, kama mbunge ni muhimu akawepo bungeni na kuisimamia serikali ipeleke maendeleo kwa wananchi.

“Mbunge anahitajika kuwepo hapa aisaidie serikali kupeleka maji kwa wananchi, kupeleka miundombinu, kupeleka madawa, na kuweka utaratibu wa kuhakikisha fedha zetu za gesi zinakaa katika mfuko maalum, wao wanakimbia. Haiwezekani,” alisema.

Maelezo yake hayo yamelenga kuwachafua wabunge wapatao 100 wanaotokana na vyama vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi, ambao waliotoka bungeni, baada ya Spika kuelekeza Kamati ya Haki ya Bunge kuwaadhibu kwa kufanya vurugu bungeni.

Wabunge hao walikuwa wanataka miongozo kwa hoja kwamba hakukuwa na sababu ya msingi ya serikali kuwasilisha miswada ya sheria kwa hati ya dharura, hasa kwa kuwa miswada haikushirikisha wananchi.

Cheyo aliyejitambulisha mapema katika bunge la 1995 kuwa ni Bwana Mapesa, akidhamiria kuwajaza mapesa wananchi, alikataa kutoka kufuata wabunge wa UKAWA wakati wa Bunge Maalum la Katiba, hivyo kubaki mpaka akapiga kura ya NDIO katika kuipitisha katiba inayopendekezwa.

UKAWA – Umoja wa Katiba ya Wananchi – ndio ulianzia hapo Bunge Maalum baada ya kubaini kulikuwa na mpango kabambe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuvuruga Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikizingatia maoni ya wananchi.

Katiba hiyo haijapigiwa kura ya maoni.

error: Content is protected !!