August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chenge kiporo cha Lema

Spread the love

 

ANDREW Chenge, Mbunge wa Bariad Magharibi, hajaponyoka mikononi mwa Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini, anaandika Happiness Lidwino.

Licha ya hotuba ya Godbless Lema, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutosomwa bungeni jana, hotuba yake ilimgusa Chenge katika sakata la rada. Kifuatayo ni kipengele hicho.

Mheshimiwa Spika,  Mh Andrew Chenge (MB) ametuhumiwa na imethibitika hapa Bungeni na katika taasisi za Uchunguzi za Kimataifa  (SFO) kuwa alihusika kwa karibu na  kwa ufanisi katika sakata la kashfa ya ununuzi wa rada ya Taifa.

Mheshimiwa Spika,  Mwandishi  Andrew Feinstein  , Colonel .U.S. Army (retired)  katika  Kitabu chake “ THE SHADOW WORLD  – Inside the Global Arms Trade, katika ukurasa wa 188-196, amefanya uchambuzi wa kina jinsi Andrew Chenge  alivyofanikiwa kukwapua fedha za Wananchi  kiasi cha pesa za Kimarekani dolari 1.2 milioni kupitia Kampuni yake ya Franton Investment Ltd  Jersey na Kampuni hii ya Andrew Chenge ikampa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Dr.  Idrissa Rashid  pesa za Kimarekani dolari $600,000 kupitia Kampuni ya Gavana huyu inayojulikana kwa jina la Langley Investment Ltd.

Mheshimiwa Spika, Lakini kwenye utawala  huu wa utumbuaji majipu, Andrew Chenge ni Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  M/kiti wa Kamati ya sheria ndogo,  jambo hili lina sura ya dharau na fedhea kwa Bunge lako tukufu na kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, Wako wengi wenye sura hizi za Mh Chenge na wengine ni Mawaziri  ambao wamekuwa na kashfa mbali mbali kwenye Serikali iliyopita lakini wameonekana kwenye madaraka tena katika Serikali hii ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais aneyeamini katika utumbuaji majipu , wakati kuna  majipu mengine asiyoweza kuyatumbua ndani ya baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, Taifa linapokuwa na huzuni  juu ya utawala  unaopuuza na kudharau Wananchi , kwa vyovyote vile hali ya amani na usalama inakuwa mashakani na kuwatia moyo watumishi wengine wa Umma katika masuala yanayohusu ufisadi, rushwa na ubadhirifu  kwamba sio mambo mabaya. Ndio maana imekuwa ni vigumu kukemea rushwa katika ngazi mbalimbali za utawala wa nchi hii ikiwemo Jeshi la Polisi.

6.2 Kuingiliwa kwa Uhuru wa Bunge na Mhimili wa Dola

Mheshimiwa Spika, tishio  lingine  la hali ya usalama Nchini  ni Serikali kuingilia Uhuru wa Bunge , ni ajabu kubwa kwamba chombo kinachopanga matumizi ya fedha za Serikali ni Bunge , lakini kwa wakati huu tumeona Serikali ikiondoa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kwa kisingizio cha kubana matumizi , kazi ambayo hata hivyo kama ingekuwa ni hoja basi jambo hilo lingefanywa na Bunge na sio Serikali.

Mheshimiwa Spika, Wananchi kupata  habari na kujua wanachojadili wabunge wao ni hitaji la lazima la Kikatiba  na sio hisani ya Serikali, malumbano yetu dhidi ya hoja mbali mbali ndani ya Bunge yalikuwa ni muhimu kwa  ustawi wa  usalama wa Nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,  Wananchi , walipotuona kupitia vyombo vya habari mbali mbali , tukilumbana juu ya maisha na maendeleo yao , jambo hili lilikuwa linasidia kupunguza tension na uchungu kwa jamii kwani walikuwa wanashuhudia tukipigana na kulumbana juu ya ustawi wa maisha yao , walipata matumaini waliposikia majibu ya Serikali hata kama yalikuwa ni uongo.

Mheshimiwa  Spika, Kambi rasmi ya Upinzani  Bungeni inasikitishwa na jinsi Bunge letu linavyoendelea kukosa nguvu na kuingiliwa na mihimili mingine ya dola kwa kuelekezwa ni kipi cha kufanywa na kipi si cha kufanywa. Ni wazi sasa bila chenga kuwa Bunge hili limeingiliwa na dola na sasa ni Bunge kibogoyo jambo linalohatarisha usalama na amani ya nchi, kwa kuwa Dola sasa inaweza kufanya chochote na isionekane kukemewa na Bunge ambalo kazi yake ni kuisimamia Serikali, badala yake sasa hivi Serikali ndio inalisimamia Bunge.

Mheshimiwa Spika, kisingizio cha gharama kubwa za kurusha matangazo ni uongo mkubwa ambao hata shetani anaushangaa, kwani hata  vyombo vingine vya habari  vilivyokuwa vinarusha matangazo ya “live” kwa gharama zao navyo vimezuiwa sio na Serikali bali na uongozi wa Bunge uliodhibitiwa na Serikali ya Dkt. Magufuli.

error: Content is protected !!