Thursday , 23 March 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Chenge, Karamagi kuwekwa kikaangoni
Habari MchanganyikoTangulizi

Chenge, Karamagi kuwekwa kikaangoni

Spread the love

RAIS John Magufuli, amepokea ripoti ya pili ya biashara ya usafirishaji wa mchanga wa dhahabu – maknikia, huku akiagiza waliokuwa mawaziri na wanasheria wakuu wa serikali zilizopita wachunguzwe, anaandika Charles William.

Maagizo hayo yametolewa leo, Ikulu jijini Dar es Salaam kufuatia kamati ya wachumi na wanasheria iliyoongozwa na Profesa Nehemiah Osora kuwasilisha ripoti yake ya uchunguzi.

Pamoja na mambo mengine, ripoti ya Prof. Osora imeeleza kuwa tangu kuanza kwa biashara ya usafirishaji wa madini mwaka 1998 Tanzania imepoteza zaidi ya Sh. 108 trilioni ambazo ni sawa na bajeti ya serikali kwa miaka mitatu, kwa makadirio ya mwaka huu.

“Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kutokana na udanganyifu wa kampuni za madini wanaoshirikiana na watumishi wa serikali wasiokuwa waaminifu,” ameeleza Prof. Osora.

“Mikataba ya madini iliyosainiwa na waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini – Dk. Abdallah Kigoda, Daniel Yona na Nazir Karamagi kwa nyakati tofauti, haikuwa na maslahi kwa taifa hili na imelisababishia taifa hasara kubwa kwa miaka mingi,” ameeleza.

Aidha kamati hiyo, imetoa mapendekezo 20 kwa Rais Magufuli ambapo imeshauri mikataba na sheria za madini ikapitiwa upya ili nchi iweze kunufaika na biashara ya madini.

Rais Magufuli akijibu mapendekezo ya kamati hiyo, amesema anakubaliana na mapendekezo yote na kwamba vyombo vyote vya dola vianze kuwachunguza watumishi wote wa serikali waliohusika katika kuliingiza hasara taifa wakiwemo mawaziri, wanasheria wakuu na manaibu wao.

“Hata shetani huko alipo atakuwa anatucheka kwani umaskini wetu ni wa kujitakia, na hii ni kwasababu ya watanzania wenzetu ambao walipewa dhamana lakini wakazitumia kuwaumiza wananchi maskini.

“Wachunguzeni wote isipokuwa huyu ambaye ametangulia mbele za haki (Dk. Kigoda), hata kama wengine ni wafanyabiashara kwa sasa kama Karamagi. Muwahoji ili tujue ilikuwaje wakaliingiza taifa kwenye hasara hii na tujue uhalali wa mali zao.

Agizo hili linamtia matatani Daniel Yona, aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini (2000-2005), Nazir Karamagi, aliyerithi nafasi ya Yona (2005-2008) huku wanasheria wakuu (AG) wa serikali zilizopita akiwamo Andrew Chenge na Johnson Mwanyika pia wakitarajiwa kuwekwa kikaangoni.

Chenge alikuwa AG wa serikali kuanzia mwaka 1993 mpaka 2005 ambapo mikataba na sharia nyingi za madini zinazolalamikiwa zilipitishwa wakati huo, huku Johnson Mwanyika akiwa AG mwaka 2005 mpaka 2008 alipostaafu kwa kigezo cha umri.

Aidha Jaji Fredrick Werema anatajwa kuwa ndiye aliyekuwa mtaalam wa sheria katika ofisi ya AG kuanzia mwaka 1984 mpaka 2007 na hivyo kushuhudia na pengine kuidhinisha mikataba hiyo. Werema ndiye aliyekuja kuwa AG baadaye (2009 – 2014).

Pia Rais amemuagiza Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria, akae na timu ya wanasheria na wataalam wazipitie upya sheria za madini ili wapeleke marekebisho ya sheria hizo bungeni huku Spika akiombwa kuitisha kikao cha Bunge hata kama ni nje ya ratiba za kawaida za Bunge.

Rais amesisitiza kuwa kampuni ya Acacia haitaweza kuendelea kuchimba madini hapa nchini na kupewa ulinzi na serikali iwapo itaishtaki Tanzania, na kwamba zuio la kusafirisha maknikia nje ya nchi bado lipo palepale.

“Eti mali ni ya kwangu, nikiilinda mtu akanishtaki na arudi aendelee kuchimba madini hapahapa na mimi nitumie polisi wetu kuwapa ulinzi huko migodini, hili haliwezi kutokea chini ya serikali yangu,” ameng’aka Rais Magufuli.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NMB yamwaga mamilioni kuimarisha afya, elimu katika Kanda ya Kati

Spread the loveBENKI ya NMB imetoa msaada vifaa mbalimbali kwa sekta za...

Habari Mchanganyiko

Mwanamke afariki akifanya mapenzi kichakani

Spread the love  Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 37 anakabiliwa na...

Habari Mchanganyiko

Taasisi ya kuendeleza uchimbaji mdogo imetakiwa kushirikiana na serikali

Spread the love  KAMISHNA wa Madini Dk. AbdulRahman Mwanga ameitaka Taasisi ya...

Habari Mchanganyiko

Almasi inayozalishwa maabara yatajwa tishio jipya kwa nchi zinazozalisha madini hayo

Spread the love  KATIBU Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amekabidhi rasmi...

error: Content is protected !!