January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chenge ajitosa kuwania uspika

Andrew Chenge

Spread the love

 

MBUNGE wa zamani wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) leo tarehe 12 Januari, 2022 amechukua fomu za kuomba uteuzi wa kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaripoti mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Chenge mwenye umri wa miaka 75, amechukua fomu hizo katika Ofisi za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo mkongwe anatajwa kuwa tishio katika kinyang’anyiro hicho kutokana na uzoefu mkubwa alionao katika kuongoza Bunge hasa ikizingatiwa kwa nyakati tofauti alikuwa Mwenyekiti wa Bunge.

Chenge ambaye alikuwa Mbunge wa Bariadi kuanzia mwaka 2005 hadi 2020, kabla ya hapo alikuwa mwanasheria mkuu wa Serikali ya awamu ya tatu nay a pili kuanzia mwaka 1993 – 2005.

Aidha, katika kinyang’anyiro hicho cha kumpata mrithi wa Job Ndugai aliyejiuzulu tarehe 6 Januari mwaka huu, tayari wanachama 17 wamejitokeza kuchukua fomu na Chenge anakuwa wa 18.

Kati ya wana CCM hao waliojitokeza ndani ya siku mbili kuanzia tarehe 10 na 11 Januari mwaka huu, wamo vigogo wa sasa wa Bunge, wabunge, wanachama wasio viongozi na waliowahi kuwa wabunge.

Job Ndugai, aliyekuwa Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu ulianza tarehe 10 na utahitimishwa tarehe 15 Januari mwaka huu, ili kupisha michakato ya ndani ya chama hicho kumpata mgombea mmoja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Msaidizi Mkuu Idara ya Oganaizesheni ya CCM Taifa, Salomon Itunda kwa niaba ya Katibu wa Oganaizesheni ya NEC, waliojitokeza ni wafuatao:

Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson na Mwenyekiti wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu.

Wabunge waliokwisha kujitokeza kuchukua fomu ni pamoja na Godwin Kunambi wa Mlimba, Emmanuel Mwakasaka wa Tabora Mjini na Joseph Kasheku ‘Msukuma’ wa Geita Vijijini.

Wengine ni, Dk Saimon Ngatunga, Tumsifu Mwansamale, Melkion Ndofu, Ambwene Kajula, Patrick Nkandi na Hamidu Chamani.

Waliowahi kuwa wabunge na mawaziri katika serikali ya awamu ya nne ni, Sophia Simba ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa Chama Cha mapinduzi (UWT) pamoka na Stephen Masele.

Masele akiwa mbunge wa Shinyanga Mjini, alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa Bunge la Afrika (PAP).

Wengine ni, Goodluck Ole-Madeve, Juma Chuma, Baraka Byabato na msomi mwenye shahada mbalimbali tisa, Profesa Handley Mafwenga.

error: Content is protected !!